Ujumbe wa Pasaka utekelezwe kwa vitendo

JANA Watanzania wote waliungana na wananchi wengine duniani katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kuitumia siku hiyo kwenda kanisani kumuabudu Mungu lakini pia kusherehekea majumbani mwao na ndugu, jamaa na marafiki.

Siku hiyo ya Pasaka husherehekewa na Wakristo duniani kwa kuwa ni nyakati ambazo mwana wa Mungu Yesu Kristo aliteswa, kufa na kuzikwa na hatimaye siku ya tatu akafufuka katika wafu.

Sikukuu ya Pasaka kwa kawaida huanzia kwa mkesha ambapo Wakristo wanasali kwa kumshukuru Mungu kwa kuwezesha kufufuka kwa mwana wa Mungu Yesu Kristo na kuimalizia asubuhi yake kwa kuendeleza maombi, kunywa, kula na kufurahi.

Katika maombi hayo ndipo viongozi wa dini hupata fursa ya kuhubiria neno la Mungu lakini pia kutoa ujumbe juu ya mwenendo mzima wa maisha ya wanadamu, ikiwemo hali halisi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi inavyoendelea.

Katika mahubiri ya jana katika sikukuu hiyo yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa dini pamoja na mambo mengi ya kuhamasisha watu kumcha Mungu, pia walisisitiza juu ya umuhimu wa kudumisha amani ya nchi, kupambana na matukio ya uhalifu na mmomonyoko wa maadili unaoelekea kuharibu sura na hadhi ya nchi.

Katika Ibada ya kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la Kristo Mfalme mjini Moshi, Askofu wa Kanisa hilo Jimbo Katoliki la Moshi, Isack Amani, ujumbe wake kwa Watanzania ni kusisitiza kuwa ni wakati sasa wa Watanzania kuungana na kuhakikisha amani ya nchi iliyodumu kwa miaka 56 sasa, inaendelea kudumu.

Askofu huyo, akabainisha wazi kuwa hali ni mbaya ya taifa kutokana na kukithiri kwa matukio ya ajabu na ya aibu, ikiwemo mauaji ya askari wanane mkoani Pwani, utekwaji na uteswaji wa wananchi, ubakaji na ulawiti, biashara ya binadamu, ulevi, matumizi na biashara ya dawa za kulevya, mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino.

Kiongozi huyo wa dini, akasema kuwa kutokana na matukio hayo ni wazi kuwa ipo haja Watanzania kuungana wakiwemo wanasiasa na kuhakikisha wanapiga vita matukio yote mabaya yanayoliharibia sifa taifa hilo, lakini pia kuhatarisha amani ya nchi hiyo.

Askofu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania, Emmaus Mwamakula, akizungumzia vitendo vya watanzania kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii, alisema imekuwa ikitumika vibaya kwa kuchafua wenzao, jambo linalojenga uhasama na chuki miongoni mwa jamii.

Viongozi wote hao wa dini walisisitizia juu ya watanzania kuweka mbele maslahi ya nchi yao badala ya kuendekeza mambo yasiyo na faida yanayozidi kulididimiza taifa hilo na maisha yao.

Ukweli ni kwamba maneno hayo ya viongozi wa dini yana uzito mkubwa na hayapaswi kupuuzwa kwani kwa kweli kipindi cha siku kadhaa zilizopita, taifa limekumbwa na misukosuko kadhaa, yakiwemo mauaji ya watu mbalimbali askari mkoani Pwani.

Pamoja na hayo, yapo matukio ya kila siku ambayo pamoja na vyombo vya dola kuyashughulikia bado yanaendelea kutokea katika jamii kama vile ubakaji na ulawiti, matumizi na biashara ya dawa za kulevya na mauaji ya vikongwe pamoja na watu wenye ualbino.

Kwa mujibu wa viongozi hao, hatma ya taifa hilo la watanzania liko mikononi mwa watanzania wenyewe, hivyo hawana budi kuhakikisha wanafanya kila wanaloweza kwa kuweka tofauti zao pembeni ikiwemo itikadi zao na kuungana kwa pamoja kudhibiti matukio hayo.

Mengi ya matukio hayo yanatokea kwenye jamii na wahusika wapo baadhi ya watu wanawafahamu, hivyo ili kufanikisha vita dhidi ya mambo hayo yanayoharibu sura ya taifa, wananchi hawana budi kushirikiana na vyombo vya dola na kuwaweka hadharani wale wote ambao wana uhakika wanashiriki kwenye matukio hayo kama viongozi hao wa dini walivyoshauri.

Ujumbe kutoka kwa viongozi hao wa dini, ni kwa kila mtanzania anayelitakia mema taifa lake, hivyo ni vyema kuweka kwanza uzalendo na kuwa makini na mtu yeyote anayehamasisha chuki, machafuko na kuigawa Tanzania.