Tatizo la maji Dar lipatiwe ufumbuzi wa haraka

MAJI ni uhai na kila mtu anajua umuhimu wake katika miili yetu. Hivyo kutokana na umuhimu huo inabidi tutunze vyanzo vya maji navyo vitutunze. Matumizi ya maji ni mengi katika maisha ya mwanadamu kwani hutumika kunywa, kupikia, kufulia, kumwagilia bustani pamoja na mengine mengi kutegemeana na uhitaji wa mhusika.

Nimejaribu kueleza umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu ili kuonesha jinsi maji yanapaswa kutunzwa. Juzi Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alikiri kuwepo kwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama katika jiji la Dar es Salaam, ambapo alisema mahitaji kwa siku ni lita milioni 510.

Profesa Mkumbo alisema hatua zinazochukuliwa sasa, zitawezesha upatikanaji wa maji kufikia lita milioni 520 na kutoa mwito kuwepo kwa usimamizi mzuri wa miradi ili ikamilike na kuanza kutumika kwa wakati uliopangwa.

Ukweli ni kwamba Profesa huyo alikiri kuwa kwa miaka 50 ya Uhuru, jiji la Dar es Salaam bado lina tatizo kubwa la maji, hali ambayo ni aibu. Nampongeza Profesa Mkumbo kwa kuona na kutambua tatizo la maji katika jiji la Dar es Salaam, kwani kwa wakazi wengi tatizo hilo limekuwa ni mwiba, hivyo kulazimisha wengi wao kunywa ama kufulia maji ya chumvi, ambayo yamefanya nguo kupauka na maji kuwa yenye kinyesi, kwa kuwa visima vingi vimechimbwa jirani na vyoo au maji machafu yaliyotuama.

Kwa hali hii, tatizo la homa ya matumbo ama kipindupindu, litaendelea kutesa baadhi ya watu kutokana na kunywa maji yasiyo safi na salama. Wakati umefika sasa tatizo la maji, liwe la historia katika jiji la Dar es Salaam kwani tatizo hilo limeacha watu wengi wakiugulia maumivu.

Pamoja na jitihada nzuri za serikali, inahitajika nguvu ya ziada katika eneo hilo la maji, kwani karibu miaka yote limekuwa likizungumzwa, lakini upatikanaji wake umekuwa ni mdogo. Kwa mfano, eneo la Mbezi Juu unaweza kuona eneo lote linapata maji bila shida, lakini ukisogea kidogo tu eneo la Goba, utabaini kuwa maji yamekuwa yakipatikana kwa watu wachache tu.

Ni kweli wananchi wa Dar es Salaam wanahamasishwa kuvuta maji, lakini ukweli ni kwamba kwa baadhi ya maeneo, maji bado yapo kwa wachache tu, kwa kuwa miundombinu yake ni ya kizamani , pia mabomba yaliyopo ni madogo, hayana uwezo wa kupitisha maji mengi. Mtu anaweza kwenda ofisi za Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) katika eneo alilopo ili kufungiwa mita kwa ajili ya kupata maji.

Lakini, huko ataambiwa kuwa eneo hilo, hakuna bomba kubwa la kuweza kufikisha maji nyumbani kwake. Matokeo yake wananchi wa jiji la Dar es Salaam, wanaendelea kuumia kwa kununua ndoo moja ya maji, ama dumu kwa Sh 400 hadi Sh 500, ama lita 1,000 kwa Sh 15,000 na kuendelea.

Ifike mahali tatizo la maji Dar es Salaam na Tanzania nzima, liishe ili watanzania wafurahie huduma hiyo ya maji. Malengo ya serikali ni kuwa ifikapo 2020, idadi ya wanaopata maji ifikie asilimia 95 ya watu wote, hivyo waziri mwenye dhamana na watendaji wakuu, wana kazi kubwa ya kuhakikisha tatizo hilo la maji linakuwa historia hapa nchini. Hivyo nguvu kubwa itumike kuwapatia wananchi maji na kuwaelimisha kuhusu kulipa ankara zao ili maisha yao yaweze kuendelea.

Naamini wizara husika ikiweka nia tatizo la maji, litakuwa ni historia kwani sasa limekuwa ni wimbo usiokwisha kwa wengi. Ni imani yangu kuwa nguvu aliyoanza nayo Profesa Kitila ikiendelea, tatizo la maji litakuwa ni historia.

Profesa Kitila pamoja na kuzungumza na wakuu wa idara wa Mamlaka ya Majisafi na Maji taka (Dawasa), wakati umefika pia wa kutoa elimu kwa wananchi wale wanaopata huduma ya maji ili waweze kulipa ankara zao kwa wakati.