Gari kugonga treni kama maumivu ya kichwa yanayoanza polepole

JUZI Jumatano mtu mmoja alikufa na wengine 23 kujeruhiwa baada ya daladala waliyokuwa wakisafiria kugonga treni katika eneo la Gerezani jijini Dar es Salaam saa 11, alfajiri. Daladala hilo aina ya Eicher lenye namba za usajili T434 DGG linalofanya safari zake kati ya Gongo la Mboto na Mnazi Mmoja, liligonga treni ya abiria iliyokuwa inatoka Stesheni kuelekea Pugu.

Tukio hili linanifanya niseme matukio ya magari kugonga treni yameanza kuwa mithili ya maumivu ya kichwa yanayoanza polepole kwani, hili si tukio la kwanza kusikika jijini Dar es Salaam. Julai mwaka jana, lilitokea tukio kama hilo ambapo daladala la kampuni ya UDA lenye namba za usajili T 696 CVP liligonga treni katika eneo la Kamata jijini humo na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine takriban 45 wakijeruhiwa.

Hii inakumbusha kuwa, maumivu ya kichwa huanza polepole na hivyo, bila kuziba ufa, tutajenga ukuta kwa kuwa ajali mbalimbali zikiwamo za majini na nchi kavu, zimekuwa moja ya maadui wakubwa wa nchi wanaochangia vifo, ulemavu na umaskini kwa jamii.

Familia na serikali kwa jumla, wanatumia rasilimali nyingi katika mazishi, kuuguza majeruhi na kuwawezesha yatima, wajane na wagane ambao wategemezi wao wanapoteza maisha katika ajali hizo sambamba na kupotea kwa nguvu kazi za familia na taifa. Hata hivyo, zipo sababu mbalimbali zinazotajwa na kubainishwa kusababisha ajali hizo hasa kwa madereva wa daladala.

Yapo mambo kadhaa yanayotajwa kuchangia ajali hizo hata matukio ya daladala kugonga treni usiku. Haya ni pamoja na madereva wa magari hayo kuchelewa kulala (kupumzika) na kuwahi kuamka hivyo, kuendelea kuwa na usingizi na uchovu wakati wa kazi. Hali hiyo, inaweza kuwa sababu ya daladala kugonga treni alfajiri. Kibaya zaidi, baadhi ya madereva licha ya kukosa sifa, pia wamekuwa na uzembe unaowafanya wajidanganye kuwa wanaweza kushindana na treni.

Ikumbukwe kuwa, kwa mujibu wa sheria za nchi na miundombinu ya barabara na reli, ajali yoyote inayohusisha treni ama iwe imemhusisha mtu, pikipiki, baiskeli au gari, ni wazi hapo treni imegongwa kwa kuwa, kwa asili yake, treni haina uwezo wa kusimama ghafla au kukwepa kama walivyo watumiaji na vyombo vingine.

Kitendo cha kuwahi kinacholenga kukusanya mapato mengi ya kutwa kwa ajili ya kuwasilisha kwa wamiliki, nacho kinawafanya madereva kufanya kazi kupita kiasi na wazembe, kuvunja sheria. Ni hatari kwamba licha ya hali hiyo kuwa hatari, bado pia wapo baadhi ya abiria wanaoshangilia mwendo kasi kwa madai ya kuwahi au, kunyamazia makosa kwa kuogopana au kutegeana.

Umefika wakati suala la kumaliza ajali likajulikana kuwa linahitaji nguvu za pamoja za jamii nzima tangu abiria, madereva na vyombo vya ulinzi maana jukumu la usalama, ni la wote. Wanapobainika wazembe wanaosababisha hali ya hatari katika vyombo vyote vya usafiri, wachukuliwe hatua kali za kisheria kwani bila hivyo, ajali zitazidi kuwamaliza Watanzania na kuwasababishia wengine ulemavu.

Kubwa zaidi, wanaobainika kusababisha ajali katika mazingira ya uzembe, wasiishie adhabu ya kulipa faini ambayo ni kiasi kidogo cha kisichowafanya wapate maumivu na kujifunza, bali adhabu itazamwe upya na iwe kali ili licha ya kuwa fundisho, pia iwe tishio halisi.

Ndiyo maana ninasema, suala la ajali zikiwamo zinazohusisha vyombo vya usafiri barabarani lisipoangaliwa kwa jicho kali, litageuka na kuwa kawaida maana, maumivu ya kichwa huanza polepole. Tuungane kukataa mazoea na ajali ili tusimchekee nyani, tukaishia kuvuna mabua.