Alichofanya JPM kwa Acacia ni busara zimpasazo kiongozi

PENYE ukweli siku zote uongo hujitenga. Rais John Magufuli (JPM) anajua kila anachokifanya na amejitoa kwa kila hali kulinda rasilimali zetu ili sote tunufaike.

Maneno aliyoyatoa wakati wa mkutano wake na Mwenyekiti wa kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Barrick, ijulikanayo kama Barrick Gold Corporation ya Canada, Profesa John Thomton, anayehusika pia na kampuni ya Acacia, ambayo Barrick ni mmiliki wake mkubwa, yameonesha kutolenga ‘kuumiza’ bali kutenda haki ili Watanzania na wawekezaji hao wafaidike.

Rais alisema kama Acacia Mining Plc itakiri makosa na kukubali kulipa fedha zilizopotea kwenye madini kwa sababu ya kuendesha shughuli zake kinyume cha sheria na kukwepa kodi, Serikali itakubali kuisajili ili iendelee na shughuli zake.

Kwa maneno hayo ya JPM, ni dhahiri kuwa aliongozwa na hekima ya hali ya juu, kwa sababu akiwa ndiye kiongozi wa ngazi ya juu zaidi nchini, angeweza kuamua vinginevyo kwa kufumba macho yake kuhusu kilichokwisha potea ilimradi asiwaone wawekezaji hao Tanzania, lakini, licha ya hatua hiyo kufikiriwa na wengi, aliona uungwana ni kuwapa nafasi waendelee kwa sharti la kurekebisha makosa na kulipa madeni.

Ni mengi yanayofanywa na Rais Magufuli yanafurahisha Watanzania, lakini katika hilo la Acacia, amezikonga nyoyo za walioufikiria uwekezaji kwa namna chanya zaidi, kwa sababu, uamuzi wake umeendelea kuwashikilia ili wawepo huku ukivutia mema kwa Watanzania, kwa kutaka wapewe chao kilichokuwa kikipotea kutokana na kutofuatwa kwa sheria na kampuni hiyo.

Hapo ndipo ninaposema JPM alitumia busara, hakuongozwa na hasira na hakutaka kutumia mabavu ambayo vile vile angeweza akayatumia kutaka waondoke zao. Rais alijua na anajua akifanyacho mara nyingi akifanya uamuzi, ingawa wanaoguswa na hata jamaa zao huwa wakitafsiri vinginevyo.

Hilo ni jambo linalonifanya nizidi kumfurahia na ninasimama hadharani katika waraka huu kusema kila kiongozi afanyapo maamuzi, afikirie mbali kama alivyofanya Rais katika suala hilo. Tunaiona sasa faida ya hatua na uamuzi wa busara wa kiongozi huyo kwa sababu Acacia imekubali kulipa fedha zote ilizosababisha zipotee kwenye madini.

Kwa Watanzania hiyo ni habari njema yenye faida. Haijalishi watalipa saa ngapi lakini ukweli unabaki pale pale wamekiri makosa na wamekubali kutulipa chetu. Asante JPM. Kadhalika, nampongeza sana Rais kwa sababu alichokuwa amesimamia sasa kinatokea.

Nakumbuka Rais amekuwa mara nyingi akisisitiza kuhusu uchenjuaji wa mchanga wa dhahabu na kusema unapofanyika nje ya Tanzania, hasara hubakia kwetu, kwa sababu wanaoyasafirisha makinikia au mchanga wa dhahabu, huficha ukweli kuhusu kiasi cha madini kilichopo.

Hilo halina ubishi kwa kuwa Watanzania tumejionea na kusikia yaliyowekwa bayana na timu ya wataalamu, waliokuwa wakichunguza kiasi cha madini katika mchanga uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya Tanzania kuchenjuliwa. Rais hakunyamaza katika hili na wapo waliopoteza nyadhifa kutokana na upotoshaji uliobainika.

Mbali na hayo, nimeona matunda ya busara za Rais kwa kutomfukuza mwekezaji huyo, hata baada ya kujua kwamba anaendesha shughuli zake nchini kinyume cha sheria na kukwepa kodi, pale yalipofikiwa makubaliano ya msingi ya kushirikiana naye kujenga mtambo wa kuchenjua madini hapa Tanzania.

Taarifa ya Ikulu ilisema kuwa makubaliano hayo yalifikiwa Jumatano iliyopita baada ya Rais Magufuli kukutana na Profesa Thomton, Dar es Salaam. Kiongozi huyo wa Barrick alisema wapo tayari kulipa kiasi chote cha fedha, ambacho Tanzania inawadai na kwamba wapo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ili kulipa fedha ambazo imepoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini.

Hongera pia kwa Profesa Thomton kwa busara alizozionesha, kwa sababu ameheshimu mamlaka kuu ya nchi yetu na Watanzania wote kwa kutotaka makuu, hivyo kukubali kumaliza tatizo kwa staili ya haki. Ninaamini utaratibu huo wa Rais kudai chetu kwa busara utatuletea wawekezaji wengi wenye nidhamu kwa rasilimali zetu. Mungu ibariki Tanzania.