Magufuli alivyotikisa usajili wachezaji nyota

DIRISHA la usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania bara lilifunguliwa juzi huku kivuli cha sera ya bana matumizi ya Rais John Magufuli ikizitesa timu zinazosajili.

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kupiga vita masuala ya rushwa, matumizi mabaya ya fedha na kusisitiza ulipaji kodi kwa taasisi na kampuni. Hatua hiyo imesababisha wafanyakazi, taasisi na kampuni zilizokuwa na matumizi mabaya ya fedha na zikikwepa kodi kulipa, kubana matumizi au kufunga biashara kabisa.

Sekta ya michezo kama zilivyo sekta nyingine za uzalishaji, nayo imejikuta ikinasa kwenye mtego wa kubana matumizi na kuathiri mwenendo mzima wa usajili wa wachezaji kwa msimu ujao.

Wakati zamani kabla hata ya dirisha la usajili kufunguliwa habari za wachezaji maarufu, nyota na mahiri zilikuwa zikitikisa hasa kwenye klabu kubwa kama Yanga, Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar, hali imekuwa tofauti msimu huu.

Hadi kufikia jana, kumekuwa na habari chache za wachezaji wenye majina makubwa kusajiliwa na timu kubwa za Yanga na Simba na kufanya usajili msimu huu uonekane hauna msisimko.

Hii inatokana na sababu nyingi, lakini moja kuu ni athari inayotokana na hatua za Rais Magufuli ‘kubana’ matumizi ya fedha na hivyo kuzuia matumizi makubwa ya fedha kiushindani.

Huko nyuma ilizoeleka kuona matajiri wa Yanga, Simba na timu nyingine wakishindana kwa kupandishiana dau wanapotaka kusajili mchezaji nyota au kuchukuliana wachezaji. Kinyume chake, mashabiki, wanachama na wapenzi wa timu hizo safari hii wanashuhudia timu zao zikisajili wachezaji wa kawaida tu.

Hii inatokana na ukweli kuwa timu hizo nazo zimepunguza mbwembwe za kusajili wachezaji nyota kwa kukosa fedha nyingi za kuwalipa. Mfano, Simba inadaiwa kumsajili kipa Aishi Manula kutoka Azam FC kwa Sh milioni 50 zinazolipwa kwa mafungu matatu ya Sh milioni 5, Sh milioni 20 na Sh milioni 25 Desemba.

Ulipaji huu wa mafungu ni ushahidi tosha wa hali ya fedha ilivyo ngumu si kwa Simba tu, bali hata Yanga, Azam na timu nyingine za Ligi Kuu. Huko nyuma kipa kama Aishi anayedakia pia timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars angekuwa ile Wazungu wanaita ‘hot cake’ na kugombewa na timu kubwa na kuongeza thamani yake sokoni.

Lakini kutokana na hali halisi, hata Azam FC, klabu yake ya zamani imeshindwa kuongeza mkataba wake ulivyoisha kwa sababu ya ukata. Ingawa Azam haikutaka kuweka wazi Aishi alitaka shilingi ngapi aendelee na mkataba, ni wazi ilimwachia kwa sababu haioni haja ya uwepo wake wakati haishiriki michuano ya kimataifa.

Azam ilikosa ubingwa wa Ligi Kuu na ule wa Kombe la FA na kupoteza fursa ya kucheza Klabu bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kutohitaji wachezaji ghali.

Hilo lilithibitishwa na Msemaji wa Azam FC, Jaffary Maganga aliyesema, wameamua kubana matumizi na ukweli kuwa hawashiriki michuano ya kimataifa hivyo kuamua kutumia muda huu, kupandisha wachezaji vijana sita wa timu yao B.

Kuwapandisha wachezaji hao kunamaanisha Azam inatumia fedha kidogo kuwasajili tofauti na kumsajili Aishi na wenzake kwa dau kubwa. Hali ni kama hiyo kwa Simba ambayo pamoja na Aishi kuwa nyota wa Taifa Stars, inamlipa fedha zake kwa mafungu kumaanisha haina fedha za kutosha kumalizana naye mara moja.

Yanga nayo ina ukata baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji kujiuzulu na kupunguza ushindani wa timu hizo kugombea wachezaji. Manji alikuwa akisajili wachezaji kwa fedha nyingi kiasi cha wengine kujisajili mara mbili na kufungiwa na Shirikisho la soka Tanzania (TFF).

Ndio maana alipojiuzulu, Yanga imeishia kusajili beki wa Jang’ombe Boys ya Zanzibar, Abdallah Shaibu Ninja ambaye kabla ya kung’ara katika michuano ya SportPesa, alikuwa hajulikani. Ingawa Yanga haijasema imemsajili kwa kiasi gani, ni wazi haitakuwa fedha nyingi kama alizokuwa anatoa Manji anapomsajili mchezaji.

Hatua za Rais Magufuli kubana matumizi iwe fundisho kwa timu zote za Ligi Kuu kubana pia matumizi yake na kuishi ndani ya uwezo wao wa kifedha ziwe na wafadhili au bila wafadhili