Wafugaji wakiwaheshimu wakulima migogoro itakwisha

HiVI karibuni Serikali iliweka bayana mpango wake kuanzisha kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kutatua matatizo ya wafugaji nchini, hususani uhaba wa maeneo ya malisho unaochangia kwa kiasi kikubwa kuzusha migogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ndiye aliyeweka wazi mpango huo akisema ataunda kikosi kazi kitakachochunguza matatizo ya wafugaji, ili Serikali iyashughulikie na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.

Samia alisema hivyo Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kuzungumza na viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania. Viongozi hao walimweleza kile wanachokiita matatizo na manyanyaso yanayowapata wafugaji nchini wanapokuwa kwenye shughuli zao za ufugaji.

Aliwahakikishia kuwa, sintofahamu inayowakumba wafugaji nchini itakwisha kwa kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na chama hicho, ambayo ni pamoja na kutengewa maeneo rasmi kwa ajili ya malisho.

Alisema, ili kujua kwa kina hali ilivyo kwa wafugaji nchini kwa sasa, Serikali itaunda kikosi kazi kitakachotembelea maeneo mbalimbali, yakiwemo yenye migogoro kuhakikisha suluhu ya matatizo inapatikana, hasa yanayohusisha wakulima.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye alimweleza Makamu wa Rais kuwa, chanzo kikubwa cha migogoro kati yao, hifadhi za taifa na wakulima ni kukosekana kwa maeneo rasmi ya malisho.

Makoye alisema ikiwa watatengewa maeneo ya malisho, hawatafuata mashamba ya wakulima wala hifadhi za taifa. Alitaka Serikali za mikoa na wilaya za Katavi na Ruvuma ziigwe kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza matatizo ya wafugaji kwa kuwatengea maeneo maalumu ya malisho.

Alipendekeza wapewe mashamba makubwa yasiyoendelezwa, ili wayageuze malisho ya mifugo, hali anayoamini kuwa itamaliza migogoro kati yao, wakulima na hifadhi za taifa. Kiongozi huyo wa wafugaji alimweleza Makamu wa Rais kuwa watakapokuwa na eneo maalumu la mifugo, itakuwa rahisi kwa wawekezaji katika sekta ya mifugo kuwaona na kuvutwa kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Alisema uwepo wao unaweza kuchochea uanzishwaji viwanda vingi vya mazao ya mifugo. Kama alivyosema Makoye, ni kweli na ninaunga mkono jitihada za Serikali kumaliza migogoro kupitia vikosi kazi inavyoviunda sambamba na umuhimu wa wafugaji kuwaheshimu wakulima.

Nakumbuka Makamu wa Rais anashughulikia suala la Mto Ruaha Mkuu kwa mtindo huo wa vikosi kazi Kwa Wazo Langu, ninaona mtindo huo unafanikiwa kwani wavamizi wa maeneo ya mto huo wanayaacha, hivyo kuruhusu ikolojia ya asili ya Ruaha Mkuu kurejea kama awali.

Pongezi kwa hilo. Hofu yangu ni kwamba, je, hatua hizo pekee zitaweza kusaidia bila wafugaji nchini kukubali kujisahihisha na kuacha kudharau kazi ngumu na muhimu ya wakulima hasa wa vijijini wanaotumia jembe la mkono?

Wafugaji wa namna hii wamekosa utu na kujaa dharau kiasi cha kuingiza mifugo katika mashamba kama kwamba hawaoni mazao au kujua kuwa yale ni mashamba. Hili, linahitaji heshima na utu.

Binafsi, naamini wafugaji pia ni binadamu wenye macho yanayoweza kuona na kutumia akili na utashi waliojaliwa kutofautisha mazao (mashamba) na majani yanayojiotea. Mara nyingi tunasikia katika maeneo mbalimbali wakulima wakiwamo wa Kilombero wakijikusanya wakiwa na silaha za jadi na kuamua kuingiza mifugo yao katika mashamba ya mahindi na mazao mengine, kisha kujiandaa kwa mapambano dhidi ya wakulima wanaokamata mifugo yao.

Kwangu mimi, njia nyingine ya kupunguza adha zinazoshawishi kulazimisha migogoro, ni ufugaji uliopitwa na wakati wa kuwa na mifugo wengi, japo wanatoa mazao kidogo. Wafugaji watambue kuwa kuuza baadhi ya mifugo na kubaki na kiasi kinachoongeza uzalishaji na tija, si dhambi wala aibu, bali ni umakini.