Upembuzi yakinifu ufanywe kunusuru barabara korofi

WILAYA ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ni moja ya wilaya zinazokabiliwa na changamoto za miundombinu ya barabara hususani barabara za ndani na kero hiyo imedumu kwa muda mrefu bila ufumbuzi.

Barabara hizo ni pamoja na ile ya Tandale, Akachube eneo la Kijitonyama, Barabara ya Mabatini na maeneo mengine ambayo yamekuwa yakifanyiwa ukarabati, lakini haudumu. Kwa mtazamo wa kawaida ni wazi ujenzi au ukarabati wa barabara hizo umekuwa ukifanywa chini ya kiwango kwani ukarabati unapoisha, haupiti muda zinaharibika kwa kiwango kikubwa.

Ubovu huo sio tu unagharimu fedha za wananchi, bali pia unaharibu vyombo vya usafiri vya wananchi, hali inayoongeza malalamiko. Swali la kujiuliza ni je, wanaopewa zabuni za kukarabati barabara hizo wana ujuzi wa kufanya kazi hizo?

Je, fedha zinazotolewa za ukarabati ni kidogo na hivyo ukarabati kufanywa kulingana na kiwango cha fedha kilichotolewa? Je, kuna uhuni unaofanywa na wazabuni hao katika kuzikarabati barabara hizo?

Hayo ni maswali ambayo huenda Manispaa au Wilaya ya Kinondoni wakawa na majibu yake, au pengine nao wasiwe na majibu kwa sababu mbalimbali zikiwemo ama kutokuwa makini katika usimamizi, au nao kuhusika kufanya udanganyifu kwa kushirikiana na wazabuni.

Kwa mfano, hivi sasa barabara ya Tandale inayoanzia eneo la Morocco Hotel hadi Sinza Kijiweni, haipitiki kabisa na imegeuka kuwa mahandaki, lakini yapo mabasi yanayofanya safari zake kwa mujibu wa sheria kutoka kituo cha Mawasiliano kwenda Msasani pia yako yanayofanya safari kutoka Makumbusho kwenda Tandika au Gongo la Mboto.

Wapo pia wananchi wanaotumia barabara hiyo kwenda kwenye makazi yao nao wamekuwa wakipata adha kubwa ya ubovu wa barabara hiyo, na wamelalamika kuharibu magari yao lakini kilio chao kinaonekana kwenda na maji.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bodi ya Mfuko wa Barabara ilisimamisha malipo yote yanayotokana na fedha za Mfuko wa Barabara kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni. Kusimamishwa huko kulitokana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na mwenendo usioridhisha wa utekelezaji na usimamizi wa miradi na kusema wataendelea na msimamo huo hadi hapo watakaporidhika na mfumo wa usimamizi wa fedha.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Joseph Haule alifikia uamuzi huo baada ya ripoti ya ukaguzi wa kiufundi kwa kazi ya ujenzi wa barabara ya Masjid-Quba yenye urefu wa kilomita 2.478 iliyopo maeneo ya Sinza Mori, inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Mradi huo ulitekelezwa na Manispaa ya Kinondoni kwa Sh bilioni 3.3 zikiwa ni fedha za mfuko wa barabara zilizotengwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kuanza utekelezaji wake Machi mwaka 2015. Mradi huo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ambayo ni Juni 16, 2015 lakini hadi Juni mwaka 2016 ulikuwa haujakamilika.

Matokeo ya ripoti hiyo yalibainisha kuwa, sehemu ya barabara iliyojengwa ambayo ni mita 700 za mwanzo, zilikuwa na upungufu katika vipimo kwa tabaka la lami lililowekwa kutokidhi viwango na hiyo ni moja ya sababu zinazofanya barabara ziharibike mara kwa mara.

Sasa hayo ni baadhi tu ya kasoro ambazo zinafanywa na wakandarasi wanaopewa zabuni kwenye ukarabati wa barabara na maswali ya kuhoji ya msingi ni kwa nini iwe kwa eneo hilo la Kinondoni?

Msimu wa mvua umeisha, barabara nyingi bado mbovu; kinachotakiwa kwa Manispaa za Dar es Salaam, ni tathmini za kina na mikakati madhubuti kuhakikisha makandarasi wenye sifa wanapatikana haraka kujenga barabara hizo kwa viwango vinavyokubalika, ili kuondoa kero na matumizi mabaya ya fedha