Simba, Yanga zisichukuliane wachezaji

HABARI ya mjini hivi sasa ni suala la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ kuhamia Simba, mahasimu wao. Uhamisho huo wa Niyonzima katika usajili kwa ajili ya Ligi Kuu ya soka Tanzania msimu ujao umezua balaa baada ya wanachama wa Yanga wanaodaiwa kuwa na hasira, kuchoma jezi yake.

Niyonzima amehamia Simba baada ya uongozi wa Yanga kuridhia kuachana naye ulipozidiwa na viongozi wa Simba, dau la kumsajili tena. Inadaiwa Niyonzima amesajiliwa Simba kwa sh milioni 130.

Viongozi wa Yanga walipanga kumpa sh milioni 80 aendelee kubaki Jangwani. Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface amekaririwa akikemea kitendo cha mashabiki wao kuchoma jezi ya Niyonzima kwa ghadhabu.

Wakati mashabiki wa Yanga wakiudhika kwa Niyonzima kuondoka, wenzao wa mtaa wa Msimbazi, makao makuu ya Simba wanafurahi. Tena ndio kwanza uongozi wao unatangaza kutaka kumchukua pia Donald Ngoma ili akaungane na Emmanuel Okwi wa Uganda.

Nilipokea habari za mashabiki wa Yanga kuchoma jezi ya Niyonzima kwa masikitiko kama alivyozipokea na kuzikemea Mkwasa. Ni kweli siku zote nafsi ya mtu huumia pale anapoondokewa au kupoteza kitu akipendacho kiwe mchezaji, mke, mtoto, mali au mzazi. Hii inatokana na uhusiano wa karibu ambao unakuwa umejengeka kati yao kutokana na undugu wa damu kati yao, ushabiki au urafiki.

Kwa mantiki hiyo, kwa mtu aliyewahi kupoteza mojawapo ya vitu hivyo, atakuwa anaelewa jinsi gani mashabiki wa Yanga walivyoumizwa nafsi. Sitaki kuwasemea mashabiki wa Yanga au Simba wanavyojisikia pale wachezaji wao wanapochukuliwa na timu pinzani kati yao.

Lakini hili la Niyonzima limenifanya nirejee nyuma kuangalia matukio kama hayo na faida itokanayo na timu hizo kuchukuliana wachezaji. Niyonzima si mchezaji wa kwanza wa Yanga kuhamia Simba ndio maana hata Katibu Mkuu Mkwasa aliwaomba wanachama watulie tu.

Vitendo vya wachezaji wa Yanga kuhamia Simba na wa Simba kuhamia Yanga kila msimu wa usajili unapofika vimekuwepo enzi na enzi. Mfano wa baadhi ya wachezaji waliohama Yanga na kwenda Simba ni pamoja na kipa Steven Nemes, kiungo, marehemu Said Mwamba Kizotta, beki Silvatus Ibrahim, Hamisi Kiiza.

Wengine ni kiungo Ezekiel Greyson ‘Jujumen’, beki Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, kipa Ivo Mapunda, mshambuliaji Clement Joseph n.k. Waliowahi kuchezea Simba na kisha kuhamia Yanga ni pamoja na Hamis Gaga, Amisi Tambwe, Emmanuel Okwi, Hassan Kessy, Method Mogella ‘Fundi’, Zamoyoni Mogella, Athumani Idd ‘Chuji’, Juma Kaseja n.k.

Orodha ya wachezaji waliohama moja kwa moja kwenda Yanga au Simba au baada ya kupita timu nyingine na kuishia timu hizo ni ndefu. Ndio maana naungana na Mkwasa kuwataka Yanga watulie kwani kuhama kwa Niyonzima si jambo geni kinachogomba ni pengo aliloacha.

Suala kubwa kwa wana Yanga kujiuliza ni kama kuondoka kwa Niyonzima kumeacha pengo ambalo haliwezi kuzibwa au linazibwa na nani. Nasema hivyo kwani hata kama Niyonzima asingeondoka leo, iko siku angeacha tu soka kutokana na umri kumtupa mkono au kuumia.

Hivyo hivyo kwa Simba au timu nyingine, hali kama hiyo inapotokea, jambo la kujiuliza ni vipi pengo linalojitokeza, litazibwa na si kukasirika. Mchezaji kama alivyo mwajiriwa yeyote, ana haki ya kuhama kwenda kwa mwajiri (klabu) mwingine kuuza ujuzi wake kwa bei anayotaka.

Na hilo lipo hata kama kuna mkataba ndio maana mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo anatishia kuondoka wakati ana mkataba bado. Cha msingi ni klabu kuishi kwa angalizo siku zote wachezaji wapo pale katika muda wakiwa wazima, wana mkataba na mapenzi na timu.

Mapenzi yakiisha hata mtu akipewa fedha kiasi gani, habadili uamuzi ndio maana Niyonzima hakubadilika licha ya Yanga kumpa milioni 80. Pengine itoshe tu kuwa fundisho kwa Simba na Yanga kuendelea kuchukuliana wachezaji bila sababu ya msingi bali kukomoana kama sasa.

Nasema hivyo nikiamini ni afya zaidi kwa klabu hizo kuchukua wachezaji wa timu zao za B na kuwapandisha au wa nje ya nchi kujiimarisha. Uzoefu umeonesha wengi wa waliosajiliwa huko nyuma hawakuwika huko walikoenda na tayari hata Niyonzima anaelezwa kuishia huko.

Kama hivyo ndivyo, ya nini kuhama wakati ukijua unaenda kuanza kugombea namba upya huku utokako ukiacha pengo lisilozibika. Hali hii ni kwa faida ya nani kama si kukomoana? Iko haja kwa Simba na Yanga kutochukuliana wachezaji ili wakuze soka la wachezaji chipukizi na kutoudhi mashabiki