Ulinzi wa watoto wakati wa sikukuu uanze kwa wazazi

SIKUKUU ya Idd el Fitr imewadia. Katika shamra shamra za kusherehekea sikukuu hii, watoto hupenda kwenda kutembea maeneo mbalimbali ya kufurahi na wenzao kama vile kwenye pembezoni mwa fukwe za Bahari ya Hindi na maeneo mengine, kama vile kwenye maduka makubwa yaani Malls.

Ni jambo zuri watoto wetu kufurahi, ila angalizo kwa wazazi ni vyema wanapowapa ruhusa watoto hao, wakawapa na mtu mzima wa kuwaongoza au kuambatana nao kwa sababu vitendo vya kuwaacha watoto kwenda wenyewe, vinahatarisha uhai wao kwa kuwa sio watoto wote watakuwa makini.

Tumeshuhudia matukio mengi ya ajali, vifo na hata kupotea kwa watoto katika sikukuu kama hizi na hiyo yote inachangiwa na wazazi kutotimiza wajibu wao wa ulinzi kwao.

Uzoefu unaonesha kwamba uwezo wa sikukuu kama hizi na nyingine za mwisho wa mwaka, huambatana na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao, ambapo baadhi ya watu kutumia vilevi kupita kiasi.

Pia matukio ya uendeshaji wa vyombo vya moto bila kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, yamekuwa yakiripotiwa kwenye vyombo vya usalama, hivyo ni vyema wazazi na walezi na jamii kwa ujumla ikachukua tahadhari ili kuwalinda watoto.

Pamoja na kuwalinda watoto hao, ni vyema wazazi na walezi wakatambua watoto wao wanaenda wapi na wako na nani kwa sababu baadhi ya watoto watukutu hutoroka au wengine kwa ridhaa ya wazazi wanaenda disko toto.

Sasa disko toto hizo sio salama kwa sababu hakuna anayeangalia maadili ya watoto hao, bali vitendo viovu vinafanyika na watoto kwa kuwa wana umri mdogo hupenda kuiga, hivyo wanaiga matendo machafu na mwisho wa siku wanaharibika na wakati mwingine kuacha masomo.

Ni vyema vitendo kama hivyo vikadhibitiwa mapema ili kuwanusuru watoto wetu na kuwajenga katika maadili mema. Ikiwezekana sio lazima msimu huu wa sikukuu watoto wako wakaenda matembezi, inawezekana kabisa familia ikawa na utaratibu wa kukaa nao na kula sikukuu nyumbani.

Iwapo kuna ulazima wa kutoka ni vyema basi ukatoka na familia yako na watoto kama ni kwenda kutembelea ndugu, jamaa au marafiki ili uwe nao iwe rahisi kuwalinda kuliko kuwaacha wazurure wenyewe jambo linalohatarisha usalama wao.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, kwa wiki kadhaa sasa ilitangaza kuwepo na upepo mkali kwenye maeneo ya bahari na maziwa, na kutoa tahadhari kwa umma kuwa makini kwani unaweza kuleta madhara.

Tahadhari hiyo inapaswa pia kuzingatiwa kwa jamii nzima, sababu michezo ya ufukweni na hasa kwa watoto wanaopenda kuogelea inaweza kuwa sio salama kwa nyakati hizi kutokana na ukweli kuwa bahari hubadilika mara kwa mara hivyo ili kuzuia maafa ni vyema watoto wanakatazwa kuogelea.

Tukumbuke kuwa kipindi kama hiki cha sikukuu, maafa mengi yamekuwa yakitokea na ndiyo maana hata jeshi la Polisi nchini, limetoa angalizo kwa jamii, wazazi na walezi kuwa makini na watoto na kuhakikisha ulinzi wa watoto unaanzia kwao.

Pamoja na jeshi hilo, kujipanga kuhakikisha usalama unakuwepo msimu huu wa sikukuu, ni vyema pia kama jamii kuchukua hatua ya ulinzi wa mali, nyumba na watoto na kuepuka matumizi ya vileo kupita kiasi kwa sababu vimekuwa vichocheo vya maovu. Nawatakia wote sikukuu njema yenye amani na utulivu!