Ni muhimu kupima afya mara kwa mara

KUWA na afya njema ni jambo muhimu na linalohitaji usimamizi wa kipekee, kwa kuwa inawezesha uzalishaji na ukuzaji wa uchumi wa nchi na hata kuongeza maendeleo. Pamoja na kwamba umuhimu huo wa kujali afya unajulikana, lakini wengi wamekuwa wakishindwa kufuatilia afya zao.

Hali hiyo inatokana na ama gharama kubwa za matibabu au wengine wanaona jambo hilo halina umuhimu hadi wanapozidiwa kwa kuumwa. Zipo taarifa za kuibuka kwa magonjwa mbalimbali, ambazo zimekuwa zikielezwa na wataalamu wa afya, huku Watanzania wakiambiwa wawe na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kutibu magonjwa mapema katika hatua za awali.

Kutokana na mazingira kubadilika, ifikie wakati uwepo msukumo wa uhamasishaji kutoka kwa makundi mbalimbali ili suala la kupima afya liwe jambo la mara kwa mara kwa watu wote ili kuepuka kukomaa kwa magonjwa ama kuwepo kwa maambukizi mengi.

Kutokana na kutopima afya mara kwa mara, watu wengi hujikuta wakipata ulemavu au hufa kutokana na kuwa na ugonjwa ambao unakuwa haukutambulika. Mambo hayo yanaweza kuepukwa kwa kusisitiza elimu ya kupima afya kusisitizwa bila kuchoka.

Ni muhimu kuwepo kwa uhamasishaji wa kupima afya kwa wananchi kama anavyosisitiza daktari bingwa wa magonjwa ya damu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Stella Rwezaura.

Mathalani, Rwezaura anasema asilimia 97 ya watanzania hawajui kama wana ugonjwa wa himofilia au hawajawahi kupima, huku asilimia tatu tu ndio wanajua hali yao kuhusu ugonjwa huo.

Kwa takwimu hizo, ni dhahiri kuwa idadi ya wasiojua kuwa wana ugonjwa huo ni kubwa mno. Hatua za haraka za kupima afya za wananchi zinatakiwa kuchukuliwa, kwa kuwa wengi wanaweza kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Ugonjwa huo unaweza usijulikane aliye nao, lakini akienda hospitali mengi yanaweza kujulikana, ikiwemo dalili zenyewe na ugonjwa kudhibitiwa mapema na mgonjwa kuepuka kupoteza maisha.

Daktari huyo anaeleza kuwa himofilia ni ugonjwa wa kurithi, lakini kwamba asilimia 30 ya wagonjwa wameupata bila kurithi, bali ni kutokana na mabadiliko ya vinasaba. Anasema ugonjwa huo ni ukosefu wa kiwango cha kutosha cha chembechembe za protini zinazotakiwa katika kugandisha damu na hivyo kusababisha damu kuvuja kwa muda mrefu, mwenye ugonjwa huo ataishi nao maisha yake yote.

Kuhusu dalili za ugonjwa huo ni kwamba mtu hutokwa na damu muda mrefu, na mgonjwa hupata nafuu baada ya kuongezewa damu au kuchomwa sindano ya chembe sahani. Ikumbukwe kuwa kuna kampeni mbalimbali ambazo hufanyika nchini kwa ajili ya kudhibiti masuala mbalimbali, kama vile tohara na hata ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike.

Hivyo, upimaji afya uwe na uhamasishaji wa lazima ili kubaini uwepo wa magonjwa, ikiwemo himofilia watu wengi hawajui kama wanao na wala hawajawahi kupima. Ugonjwa huu unapaswa kufanyiwa uhamasishaji ili watu waweze kuufahamu, kwa sababu kwa uwiano kwa mujibu wa Dk Rwezaura, katika kila watu 10,000 mtu mmoja ana ugonjwa huo.

Hivyo, kwa hapa nchini inakadiriwa kuna wagonjwa 5,400 wa himofilia, lakini waliojiandikisha kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni 100 tu. Idadi hiyo ya wagonjwa ni ndogo mno, ukilinganisha na idadi kamili ya waliopo. Kwa ujumla, hali hiyo inaonesha kuwa wananchi wengi hapa nchini hawaoni umuhimu wa kujali afya zao mapema, badala yake husubiri hadi wakiwa wamezidiwa.