Mambo kama haya si ya kufumbiwa macho

JUZI kuna taarifa zilieleza kwamba Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa, Bernard Makali kuunda timu itakayochunguza sababu za Wilaya ya Nkasi kuficha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Inadaiwa kwamba walikuwa wakiwatibu wagonjwa kimya kimya huku mkuu huyo wa mkoa akiagiza pia msako kubaini wanaowatibu nyumbani kwa siri. Habari kama hii ni ya kusikitisha na kuhuzunisha kwa sababu wahenga husema mficha maradhi kifo humuumbua.

Kwa hali ya kawaida kabisa unaposikia mtu anaumwa halafu anaficha ugonjwa unamuhurumia kwa kuwa mwisho wake huwa si mzuri kwa kuwa ugonjwa unaweza kumuathiri kisaikolojia na wakati mwingine kumsababishia mauti wakati kama angeweza kujitokeza mapema angeweza kupata ushauri na tiba kutoka kwa wataalamu na akapona.

Sasa tunaposikia kwamba kuna sehemu kuna wagonjwa wa kipindupindu na wanafichwa na kutibiwa kisiri ni jambo la kuogopwa kwa sababu hata namna na kujihami na kujikinga kwa majirani inashindikana.

Tunafahamu kwamba unapotokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hatua za haraka huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandaliwa au kutengwa eneo maalumu kwa wagonjwa na hii hutokana na jinsi ugonjwa huo ulivyo na athari za haraka kwa jamii.

Yawezekana ugonjwa wa kipindupindu nchini unaonekana kama mazoea na baadhi ya watu kutoupa uzito ila ukweli ni kwamba ugonjwa huo umekuwa ukiteketeza Watanzania wengi pale unapolipuka. Chanzo kikubwa cha ugonjwa huu huletwa na vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu.

Kwa miaka mingi sasa baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakikumbwa na magonjwa ya aina mbalimbali ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa kipindupindu ambao huenea kwa kasi kubwa pale unapoibuka kutokana na kuwepo kwa mazingira hatarishi yanayochochea mlipuko wa ugonjwa huo.

Pia kutozingatia usafi wa mazingira, vyakula, maji, pamoja na kinga dhidi ya ugonjwa hatari wa kipindupindu husabisha kurejea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Kutokana na hali hiyo pia Zelothe ametaka watakaobainika kuwatibu wagonjwa hao kwa siri wachukuliwe hatua kali za kisheria haraka huku akisema kufichwa kwa ugonjwa huo kumesababisha taratibu za kuudhibiti kutofuatwa hivyo kusababisha watu wengi kushambuliwa na ugonjwa huo na hivyo kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Mkuu wa mkoa alitoa agizo kwa RAS kufuatia kifo cha Salvatory Kayumba (60) kilichotokea mwezi Mei mwaka huu. Inasemekana alikufa kwa ugonjwa huu huku chanzo cha mlipuko wa ugonjwa huo ikiwa ni maji ya kisima kiitwacho Namanyoro ambapo wakazi wa Kijiji cha Mpasa walikuwa wakiyatumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kunywa.

Hali kama hii si ya kufumbiwa macho na kama ni kweli hili lipo ni jambo la kuangaliwa kwa umakini mkubwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Haiwezekani ugonjwa kama huo ambao kila mtu anafahamu hatari yake ukafumbiwa macho au ukatibiwa kwa siri wakati unatakiwa kuwekwa bayana ili wananchi na vyombo mbalimbali wachukue tahadhari.

Sote kwa pamoja tunatakiwa kutoa ushirikiano pale unapotokea jambo ambalo si la kawaida au mlipuko wa magonjwa ili hatua za kukabiliana nayo pia zipangwe kwa pamoja. Kutokana na hali hiyo ni vyema sasa viongozi wote wa serikali wa Mkoa wa Rukwa pamoja na wadau mbalimbali kushirikiana ili kuhakikisha wanakabiliana na ugonjwa huu na kuokoa maisha ya wananchi