Tusitafute magonjwa tukijivunia bima

KILA mmoja ni mgonjwa, mwenye ulemavu au maiti mtarajiwa. Hakuna ajuaye siku wala saa ambayo lolote kati ya hayo au yote, yatamfika; hiyo ni siri ya Maulana. Mwanamuziki Mbaraka Mwishehe katika wimbo uitwao, “Shida” anasema shida haina ngoja ngoja na mahali popote shida hutokeza; haichagui mtu, siku wala mwaka; kwa maskini na matajiri wote ni shida.

Kimsingi, shida yaweza kuja wakati wa raha au wakati unapokuwa umezongwa na shida nyingine hivyo, ikawa shida juu ya shida. Ndiyo maana mifuko ya jamii imeanzisha mafao mbalimbali yakiwamo mafao ya matibabu ili kusaidia kupunguza mzigo kwa wanachama wao yanapotokea majanga.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF, unasema lengo la mafao ya matibabu ni kumkinga mwanachama dhidi ya janga la maradhi na upungufu wa kipato unaoweza kutokana na gharama za matibabu.

Katika banda la Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, mmoja wa maofisa wa NSSF ambaye hakutaka kutajwa gazetini anasema, akirejea moja ya vipeperushi kuwa, “Lengo lingine ni kutimiza matakwa ya kisheria kama yalivyoanishwa katika Sheria ya NSSF Na. 28 ya Mwaka 1997.”

Licha ya kutaja sifa za mwanachama anayestahili kunufaika na mafao ya matibabu, pia anazitaja huduma ambazo mfuko hauhusiki nazo katika mafao ya matibabu kwa wanachama na wategemezi kisheria.

Hizi ndizo kini cha Wazo Langu ili kama mambo haya yakieleweka vizuri, basi hata malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu kuhusu mafao ya matibabu katika mifuko ya hifadhi ya jamii na bima, yatapungua na kadhalika, afya ya jamii itaimarika kwani mengi yanatokana na watu wengi kutokujua kanuni na taratibu.

NSSF katika machapisho yake inataja huduma zilizo nje ya mpango kuwa ni pamoja na zile zinazotolewa kupitia mpango wa Serikali kama VVU/Ukimwi, ukoma, saratani (kansa), magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, huduma za afya kwa mama na mtoto, chanjo, kifua kikuu na kisukari.

Wazo Langu limegundua kuwa, yapo magonjwa au huduma kadhaa zisizotolewa kwa mpango huo ambazo kwa kutokujua, zimewafanya baadhi ya watu kulalamika yakiwamo magonjwa ya kujitakia ambayo kimsingi, mfuko unasema hauhusiki kuyahudumia kwa mteja au mwanachama wake na wategemezi wanaonufaika na mafao ya matibabu.

Ofisa huyo anasema, “Mpango huu hauhusishi madhara yatokanayo na kushiriki mambo au mikusanyiko isiyo halali kisheria au yenye sura ya uhalifu kama vile maandamano na migomo.”

Anasema, “Hata kama ni mwanachama, ukijihusisha na mambo hayo na mengine ambayo ni kinyume cha sheria mathalani wizi, NSSF haiwezi kukupa mafao na ndiyo maana kwa kutoyajua hayo, baadhi ya watu wamekuwa wakidhani kuwa taasisi zinazohusika zinawafanyia roho mbaya…”

Magonjwa ya kujitakia ambayo katu hayahusishwi katika mipango hii ni pamoja na madhara yatokanayo na athari za ulevi wa pombe, dawa za kulevya, matumizi ya sigara na jaribio la kujiua au utoaji mimba usio halali.

Kwa wazo langu, mifuko hii inaona mbali na hivyo, ni wajibu wa kila mwanachama au mnufaika wa mafao ya matibabu, kuepuka vitu au mambo yasiyo ya lazima, yanayokwenda kinyume na maadili ya jamii na sheria za nchi, ambayo pia ni hatari kwa mtu mwenyewe na jamii inayomzunguka.

Kwa mfano, jaribio la kujiua au kutoa mimba, pamoja na madhara mengine ya kujitakia kama kutumia mwili kufanyia majaribio ya dawa na kemikali mbalimbali, ni mambo hatari yasiyopaswa kuchekewa hivyo, mtu anapoyanya, ajue anachuma janga kwa makusudi.

Ndiyo maana ninasema katika Wazo Lango, tuache matatizo yaje yenyewe tukabiliane nayo kwa nguvu na umoja, lakini tusiyatafute kuyaleta eti kwa kuwa, kuna mafao ya matibabu mambo yakiharibika