Uandaliwe mwongozo kudhibiti ujangili

PAMOJA na jitihada zinazofanywa na wadau wa maliasili, uhalifu dhidi ya wanyamapori na misitu umebaki kuwa changamoto kubwa nchini. Tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 60.3 kati ya mwaka 2009 na 2014 kutokana na ujangili.

Kukithiri kwa uhalifu huo kunalazimisha wadau kubuni njia mpya kupambana na hali hiyo kwa kurekebisha na kuweka mwongozo wa upelelezi na uendeshaji wa mashitaka ili kupata matokeo bora.

Mwongozo huo ambao umeandaliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) umezinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, unaweka viwango na utaratibu unapaswa kufuatwa katika hatua zote za upelelezi na uendeshaji wa mashitaka.

Kwa kuwa kumekuwa na ushirikiano mdogo baina ya waendesha mashitaka, wapelelezi na vyombo vya dola vyenyewe, mwongozo huo umekuja kwa wakati mwafaka kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano ili uhalifu wa wanyamapori na misitu ukomeshwe.

DPP na wadau wengine wanalenga kuhakikisha kuwa kesi hizo zinapelelezwa na kuendeshwa vizuri na kutaifishwa mali zinazohusiana na uhalifu huo.

Mara nyingi, kumekuwa na athari za moja kwa moja zinazosababishwa na uhusiano hafifu ikiwemo upelelezi kufanyika bila kuzingatia masuala mtambuka kama vile uchunguzi wa kifedha, rushwa, utafutaji na ukamataji wa mapema wa mali zilizotokana na uhalifu, ukusanyaji wa ushahidi toka nje ya nchi, kutozingatiwa kwa mambo ya kisheria wakati wa ukusanyaji wa ushahidi na kutopelekwa mahakamani.

Nimpongeze DPP kwa kuona kwamba ipo haja ya kuwepo kwa mwongozo huo unaowataka wadau wote kutimiza wajibu wao ipasavyo kwani kumekuwa na mapungufu mengi yanayosababisha kushindwa katika kesi hizo.

Changamoto ya kutokuwepo kwa mwongozo juu ya uandaaji wa mpango wa upelelezi na uendeshaji wa mashitaka, maandalizi hafifu ya mashahidi, vielelezo na mawasilisho hafifu ya hoja ya adhabu umechangia upande wa pili wa washitakiwa kutumia makosa hayo na kumpatia faida mshitakiwa kwa kuachiwa huru hata kama ana kosa.

Mwongozo huu uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kwani hauwezi kupata matokeo chanya katika kupambana na uhalifu kama hautajipanga kwa namna gani utafanya ili kuhakikisha wale wote wenye makosa wanatiwa nguvuni.

Pia, suala la dhamana lililozungumziwa katika mwongozo huu ni la msingi kwani kupatiwa dhamana kwa washitakiwa hao na kisha kutoroka, husababisha kesi kutoendelea na serikali kukosa mapato au haki yake.

Kwa kuwa masuala haya ya wanyamapori yanagusa sekta nyingi ikiwemo mahakama, wanapaswa kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Samia Suluhu kwani mwongozo wao unapaswa kulenga katika utoaji adhabu.

Alisema katika mahakama itasaidia mahakimu na majaji kutoa adhabu na dhamana zinazowiana kwani mara kadhaa imejitokeza majaji na mahakimu kutoa adhabu zinazotofautiana au masharti yanayotofautiana katika kesi zenye mazingira sawa.

Hivyo, mahakama kama mdau wanapaswa kuona umuhimu wa kuwapatia watumishi wake mwongozo ili kuwepo na uwiano katika utoaji adhabu na masharti. Naamini mahakama itakapoandaa mwongozo itasaidia kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya wahalifu wa wanyamapori wanaokaribia kutoweka Tanzania na itawatia hofu wahalifu wapya wanaotaka kujiingiza katika masuala hayo.

Kwa kuwa mahakama ndiyo yenye kuhukumu, ni wazi itaona umuhimu wa kuwa na mwongozo ili kuwalinda wanyamapori kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.