Watanzania tushikamane kulinda rasilimali

NIANZE moja kwa moja kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa mikakati yake ya kuhakikisha rasilimali za nchi hazipotelei mikononi mwa wachache, wala Tanzania haiishii kuwa daraja la kupitishia mataifa mengine kuelekea utajiri, huku Watanzania tukibaki ombaomba.

Nchi yetu Tanzania ndiye mama wa kila Mtanzania, akiwemo Rais mwenyewe, hivyo sote tunapaswa kumpenda mama huyo na kupenda mazao yake ambayo ni pamoja na rasilimali zake kama madini ya aina zote, misitu na mazao yake, mito, maziwa, bahari na mazao yake.

Miongoni mwa maeneo na rasilimali za Tanzania ambazo Watanzania hatuna budi kuhakikisha tunaungana kuzilinda, ni pamoja na mbuga za asili na wanyama waliopo na vivutio vingine, mazao ya bahari na maziwa kama samaki na vivutio vingine vya utalii kama Mlima Kilimanjaro; bila kusahau madini.

Kadhalika, nawapongeza wananchi wanaosimama kidete kuwafichua wanaofuja rasilimali za nchi nikisema wazi kuwa, wanachokifanya hao ni uzalendo unaostahili kuigwa na kila mmoja, badala ya kulaumiwa wala kubezwa.

Kwangu mie, awezaye kusimama na kusema kama alivyosema Rais John Magufuli wakati akikemea wizi dhidi ya rasilimali za nchi sasa basi, ndiye huyo tunayepaswa kushirikiana naye huku tukimwita shujaa wetu wa karne.

Takwimu zinaonesha kuwa, kwa mwaka mmoja, wastani wa pato la taifa la Sh bilioni 18.3 linatokana na mbao zinazovunwa kwa kufuata utaratibu ikiwemo kulipiwa kodi halali kwa Serikali.

Ndiyo maana ni vema hata kujiuliza kuwa ni mara ngapi tumeshiriki ama kwa kufanya hivyo wenyewe, au kuwafichia siri majangili wa maliasili hizo tukiwaacha waendelee kuvamia misitu, kuichoma na kuteketeza uoto wa asili huku wengine wakiiba miti kwa kuikata bila mpangilio na kujinufaisha wenyewe au na familia zao.

Ukiachilia mbali faida zilizo wazi za madini na utalii nchini, bado pia utunzaji wa mazingira ikiwamo misitu una faida nyingi ambazo katu hatupaswi kuzifanyia uzembe zitoweke. Hizi ni pamoja na zile za kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuchangia pato la taifa kutokana na uvunaji halali na pia, kutengeneza ajira.

Mfano mzuri wa rasilimali ni mashamba ya serikali ya miti ambayo takwimu zinaonesha kwa mwaka 2016/17 yalivunwa na kuuzwa. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani, miti hiyo iliuzwa katika viwanda vya kuzalisha mbao na kuipatia Serikali Sh bilioni 55.1 ambazo ni mrahaba na tozo, ushuru wa halmashauri za wilaya na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Aidha, mashamba hayo katika kipindi cha mwaka 2015/16 yaliingizia Serikali Sh bilioni 58.3 kutokana na kuvunwa meta za ujazo 767,946.46. Ni kwa msingi huo ninasisitiza kuwa, kila mmoja awe mlinzi wa rasilimali za ncghi na Yule anayefanya hivyo, apewe pongezi na shukrani kwa kutimiza wajibu wa kizalendo.

Ili kulifanya vema na kufaidi matunda yake, lazima Watanzania tushikamane kulinda rasilimali zetu. Kila mmoja aseme, “Ufujaji na wizi wa rasilimali za nchi sasa basi."