TRA ifuatilie wenye EFDs wasiotaka kuzitumia

WAKATI Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiendelea kusisitiza wafanyabiashara waliofi kia kigezo cha kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) wazitumie na kuwapa wateja wao risiti zinazotokana na mashine hizo, wapo wanaozihodhi lakini hawazitumii.

Uamuzi wa Serikali kuanzisha matumizi ya EFDs ulitokana na nia yake ya kutaka kuongeza makusanyo ya mapato, kwa kuwa zinapotumika mashine hizo, uwezekano wa kupotea kwa miamala ya manunuzi iliyorekodiwa kielektroniki ni sifuri, labda kama mashine zitakuwa na kasoro.

Nakumbuka wakati fulani iliwahi kuripotiwa kuwa baadhi ya mashine za EFDs zina kasoro, lakini haikuchukua muda mrefu kasoro hizo zilirekebishwa na mamlaka husika.

Tumeona jinsi mapato yanavyoongezeka kila wakati, tofauti na kipindi cha miaka ya nyuma ambapo wafanyabiashara walikuwa wakitumia risiti zilizoandikwa kwa mkono na kuamua kupunguza au kuongeza kiasi cha fedha zilizolipwa katika manunuzi husika.

Utaratibu huo ulitoa mwanya mpana kwa wafanyabiashara wengi wasio waaminifu kuiibia Serikali fedha walizopaswa kuilipa, ikiwa ni kodi ya mapato kwa ajili ya huduma za jamii. Kwa sasa, TRA pamoja na kuelimsha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutoa na kudai risiti katika kila biashara halali inayofanyika ikiwa na faida inayomstahili mfanyabiashara kulipa kodi ya Serikali, inaendeleza kampeni ya kukagua biashara mbalimbali kuona endapo wahusika wanatumia mashine hizo za EFDs.

Kampeni hiyo imekwishavifikia vituo vya mafuta ambapo, 710 vilifungiwa ili kuhakikiwa kama vinatumia mashine hizo au la. Kati ya hivyo, 469 vilifunguliwa baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na mamlaka hiyo ya mapato, ambavyo ni kulipia gharama za ufungaji EFDs kwa mawakala walioidhinishwa na TRA kisha kuingia makubaliano ya muda maalumu ya kuhakikisha mashine hizo zimefungwa.

Kigezo kingine ni kufunga mashine za EFPP kwa waliokwishanunua, ambao hata hivyo hawajazifunga au waliozifunga mashine hizo lakini hawajaziunganisha na pampu zao za mafuta.

Inaelezwa kuwa hadi sasa vituo 241 havijafunguliwa kwa sababu ya kushindwa kukidhi masharti ya TRA. Ikumbukwe kuwa Rais John Magufuli aliamua kuiongezea Serikali jukumu la kuhakikisha watoto wetu wanasoma bure kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari, akiamini kuwa Tanzania ina wafanyabiashara wengi na makundi mengine ya watu wenye uwezo wa kugharamia huduma hiyo ya jamii kupitia kodi.

Hatua hiyo ya Rais itakuwa na mafanikio iwapo kila anayepaswa kulipa kodi atalipa. EFDs zinakusaidia hata unayezikimbia kwahiyo usizikwepe, zitumie.