Tuwe wazalendo kwa kutumia vya kwetu

JUZI Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati akizindua huduma za kifedha za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL PESA), aliwataka wananchi kuonesha uzalendo kwa kutumia mali na bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Ni kweli kwamba kwa muda mrefu sasa, wananchi wengi tumekuwa tukipenda kutumia na kuagiza bidhaa kutoka nje, badala ya kutumia vitu au bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini kwa kuogopa gharama au kwa kisingizio cha ubora.

Hata katika maisha yetu ya kawaida, tumekuwa tukitumia bidhaa nyingi kutoka nje kila siku kuliko kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini huku tukilalamika kwamba soko letu halikui.

Wakati tukikazana kununua bidhaa kutoka nje, pia tunasahau kwamba sisi tuna soko linalostahili kukua na pia tunatakiwa kukuza viwanda vyetu ili vizalishe zaidi kwa ajili ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

Tukiwa tunaelekea katika uchumi wa viwanda ni lazima wote tufunge mkanda na kuhakikisha kwamba tunavipenda vya kwetu ili kuviunga mkono viwanda vyetu pamoja na wajasiriamali wetu ili waweze kuzalisha zaidi.

Tanzania imekuwa na viwanda tofauti vikiwemo vya kuzalisha nguo, viatu na bidhaa za vyakula. Lakini pamoja na hayo, bado kuna bidhaa nyingi za aina hiyo hiyo kutoka nje huingizwa na hutumiwa kwa wingi kuliko za ndani.

Vipo viwanda vingi ambavyo vimekuwa vikitengeneza bidhaa bora za ngozi, vikiwemo viatu vya uhakika, lakini wananchi bado wanakimbilia vinavyotoka nje. Zipo pia nguo za mitumba zikiwemo za ndani, ambazo zimekuwa zikitumika kwa wingi pamoja na kupigwa kwake marufuku, hivyo ni wakati sasa wa kusimamia sheria na taratibu sambamba na kuelimisha umma kuwa wazalendo kwa kupenda vya kwetu.

Mbali na hivyo, pia wajasiriamali wetu wamekuwa wakijitahidi kubuni mbinu mbalimbali za biashara, lakini wateja wakubwa wanaotegemewa huagiza bidhaa kutoka nje na hivyo wajasiriamali wengi, kujikuta wakikata tamaa ya uzalishaji.

Kwa kuwa sasa kuna malengo hayo ya kuingia katika uchumi wa viwanda, ni vyema sasa zikawekwa juhudi ili kuhakikisha bidhaa zinazotumiwa kwa wingi ni za ndani ili kuinua wajasiriamali wetu, wafanyabiashara na viwanda vyetu.

Lazima tukubali kupenda vya kwetu ili tuweze kupiga hatua ya maendeleo kwa kuwa ili tuingie katika uchumi wa viwanda ni lazima juhudi zionekane katika kuwekeza kwenye viwanda na kutumia kwa wingi bidhaa zinazozalishwa.

Tukumbuke kwamba tunaponunua au kutumia bidhaa za ndani, tunakuwa tumechangia uchumi wetu na pia tunakuwa tumenyanyua ndugu zetu kiuchumi. Tudumishe uzalendo kwa kutumia bidhaa zetu zinazozalishwa nchini.