Tujifunze kwa Everton

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara umepangwa kuanza Agosti 26 mwaka huu, ambapo jumla ya timu 16 zitapambana kuwania taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Yanga.

Ratiba ya ligi tayari imewekwa hadharani na kila timu inamfahamu mpinzani wake itakayeanza naye katika mbio hizo za kuwania ubingwa. Ligi Kuu ya msimu huo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na usajili mzuri wa wachezaji ambao umefanywa na timu nyingi.

Kwa sasa timu nyingi zipo kwenye kipindi cha usajili, lengo likiwa ni kuimarisha vikosi vyao ili viweze kufanya vizuri katika kuwania ubingwa. Itapendeza kama usajili huo utaonesha msisimko kama ambavyo wadau wengi na mashabiki wa mchezo huo wanavyotarajia.

Imekuwa kawaida kila msimu ushindani ni kwa timu chache kubwa za Simba, Yanga na Azam. Wadadisi wa soka wanasema kinachochangia timu nyingine kutofanya vizuri ni kukosa maandalizi ya kutosha na hivyo timu nyingi zimekuwa zikifanya maandalizi ya zimamoto na kujikuta zikiwa wasindikizaji kwenye ligi hiyo.

Kwa mpango huo, ligi haiwezi kuwa na mvuto na hapo hata malengo ya kuwa na timu bora ya taifa hauwezi kufanikiwa kwa sababu hizo. Kwanza ligi yenyewe ni fupi hivyo wachezaji wanacheza mechi chache ambazo kitaalamu hazitoshi kumweka mchezaji fi ti kiasi kikubwa.

Maandalizi yanayozungumziwa hapa siyo yale ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Uhuru au pale Kaitaba Bukoba. Timu zinapaswa kusafi ri kwenye nchi nyingine ili kupata muda wa kutosha kujiandaa kwa msimu mpya.

Hivi karibuni nchini kwetu tulikuwa na ugeni wa timu ya Everton kutoka England. Everton haikuja kutembelea mbuga za wanyama tu Ngorongoro, bali walikuja kwa lengo la kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi yao inayotarajiwa kuanza katikati ya Agosti.

Hongera kwa klabu za Simba na Azam ambazo zimetambua umuhimu wa maandalizi kwani zimeondoka nchini na kwenda kupiga kambi nchi za nje kujiandaa na ligi hiyo wakiwa na lengo la kuleta upinzani wa kweli katika ligi.

Simba imekwenda kujichimbia Afrika Kusini kufanya maandalizi wakati Azam ilienda Rwanda ambako ilijifua huko kwa wiki tatu kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Huko nyuma mabingwa watetezi Yanga, walikuwa na kawaida ya kwenda Uturuki, kujiandaa na msimu mpya lakini msimu huu wamekuwa kimya pengine kutokana na ukata. Kwa kuwa timu hiyo ni kubwa na inashiriki michuano ya kimataifa, itapendeza kama itaendelea na utaratibu wake wa kwenda nje.