Umakini unahitajika kuchagua kozi sahihi

IKIWA ni wiki mbili zimepita tangu Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) litangaze matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2017 huku asilimia zaidi ya 97 ya wasichana wakifaulu mtihani huo, ni wakati mzuri sasa kwa wazazi na walezi kuwashauri vyema masomo ya kuchukua, wanapoomba kujiunga na elimu ya juu.

Mara nyingi tumeshuhudia wazazi wakiwachagulia watoto wao nini cha kusoma, jambo ambalo wakati mwingine sio sahihi kwa sababu atasoma tu kwa vile mzazi kasema na sio fani anayoipenda.

Kwa kuwa mwaka huu, mfumo wa kudahili vyuoni umebadilika, ambapo wahitimu wataomba moja kwa moja nafasi za masomo kwenye vyuo wavipendavyo kulingana na sifa zao, ni vyema umakini ukatumika kufanya chaguo sahihi ya fani hizo.

Nasema hivyo kwa sababu awali wengi walikimbilia kuomba kusoma fani za elimu, kwa vile tu waliochaguliwa walipata fursa za kupewa mkopo kwa asilimia 100, hivyo wakaona ni bora kusoma fani hiyo kwa kigezo cha kupewa mkopo.

Tufahamu kuwa kila mmoja anapenda fani fulani, hivyo ni wakati muafaka sasa ambapo vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vimetangaza nafasi za masomo na kutoa vigezo vya kila fani, wahitimu wenye sifa wakachagua masomo wanayoyapenda ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye fani husika.

Tukumbuke kuwa ikiwa umesoma fani unayoipenda, ni wazi kwamba hata ulichosomea utakifanya kwa moyo, kwa maana ni kitu unachokithamini na wala hukulazimishwa kusomea.

Wazazi na walezi tuwe makini kwenye hili la kuwachagulia watoto wetu fani za kusoma. Ingawa ushauri ni muhimu, lakini mapenzi ya fani uipendayo, kamwe usifikirie na mwanao ataipenda.

Mpe nafasi na yeye akuambie fani apendayo, kisha jadilianeni na kufikia muafaka. Hivyo, wazazi, walezi na hata washauri ni vyema mkatumia nafasi zenu vizuri, kushauri na sio kuwachagulia watoto nini cha kusoma. Wapeni nafasi wakuelezeni wanachokipenda.