Usalama kazini muhimu kwa wafanyakazi

USALAMA wa wafanyakazi katika mahali pao pa kazi ni jambo muhimu kwa waajiri ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima kazini. Waajiri wanapaswa kuzingatia kwamba mfanyakazi anapofanya kazi katika mazingira salama inamsaidia kuepuka madhara ya mwili kwa urahisi.

Wafanyakazi wanaojihusisha na kazi za ujenzi wa majengo, barabara, migodini, viwandani, usambazaji wa mabomba ya maji na nyaya za umeme wana uwezekano mkubwa wa kuumia au hata kupoteza maisha kutokana na aina ya kazi na vifaa wanavyotumia ikilinganishwa na wafanyakazi wa ofisini.

Wafanyakazi wa ofisini wanaweza kuwa kwenye hatari zaidi endapo mfumo wa umeme wanaoutumia katika vitendea kazi vyao kama kompyuta, mashine za fotokopi au printa haujafungwa vizuri, hivyo inaweza kusababisha mlipuko kwa vifaa hivyo kutokana na hitilafu ya umeme na kuleta madhara kwa mhusika au wahusika.

Nilipotembelea shughuli za ujenzi wa barabara za juu Tazara, nilishuhudia wafanyakazi wakiwa katika mavazi maalumu ya kazi kama vile kofia ngumu, viatu aina ya buti na vikoti vya kung’aa ili kuwawezesha kuonana kwa urahisi lakini pia kuepuka kujeruhiwa na vyuma au mbao au nondo na vitu vyenye ncha kali.

Meneja wa Mradi wa barabara za juu Tazara, Nobuhiko Maruni, amesema kwamba tangu mradi huo uanze Desemba mwaka 2015, wameweza kufanya kazi bila mfanyakazi yeyote kuumia au kupata madhara yoyote kwa kumbukumbu alizonazo hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.

Alisema kwamba Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Limited imeweka utaratibu wa kuwa na mikutano ya muda mfupi kila siku asubuhi kabla ya kazi ili kuwakumbusha na kuzidi kuwaelimisha wafanyakazi wao umuhimu wa kutumia vifaa vya kazi ili kujikinga na madhara ama ya kuangukiwa na vyuma au mbao au nondo au kitu chochote ambacho kinaweza kuwaumiza au hata kuhatarisha uhai wao.

Kampuni hiyo kutoka nchini Japan, inaona fahari wafanyakazi wao kuzingatia mafunzo ya usalama kazini wanayowapatia lakini pia inaongeza ufanisi wa kazi kwa kuwa hakuna ajali zilizotokea kwa takribani miezi 19 sasa tangu ujenzi uanze.

Swali linabaki, hali ikoje hapo kwenye eneo lako la kazi? Nikitazama nyuma na kuangalia baadhi ya makampuni niliyowahi kufanya nao kazi, hali ya usalama kwa wafanyakazi ilikuwa mbaya.

Ukiacha mbali kupatiwa vifaa vya kazi, lakini hata maji ya kunywa yaliyo safi na salama ni ngumu kuyapata. Afya na usalama wa mfanyakazi awapo kazini ni jambo linalopaswa kusimamiwa kwa nguvu zote na mamlaka husika zilizopewa jukumu hili kisheria kwa kuwa baadhi ya waajiri hawajali afya na usalama wa wafanyakazi wao wawapo kazini.