Watanzania tuiombee Kenya iwe na uchaguzi wa amani

WATANZANIA tumebahatika kuwa katika nchi yenye amani, kiasi cha kuyavutia mataifa mbalimbali ulimwenguni na kukuza utalii wetu. Inawezekana ni kwa sababu ya kupenda kwetu amani, Mungu ameamua kuiacha iendelee kuna kwetu.

Hilo linawezekana pia kwa sababu Watanzania tumekuwa na utaratibu wa kuomba amani kwa ajili ya nchi yetu. Imeandikwa katika vitabu vitakatifu vya Mungu kuwa lolote tuliombalo kwa imani katika sala zetu tutapokea.

Siku zote Mungu amekuwa mwaminifu kwa Tanzania kwa sababu watu wake, bila kujali dini wala kabila wamekuwa wakifanya maombi maalumu kwa ajili ya nchi na viongozi wake.

Kwa maana hiyo, ikiwa tumeweza kuomba kwa ajili ya nchi yetu na Mungu akatenda mema kwa kuendelea kuilinda na kuitunza amani yetu, je haiwezekani tukawaombea na jirani zetu kwa imani ili wawe na amani hasa katika kipindi cha uchaguzi?

Imeandikwa katika vitabu vya Mungu kuwa aombeaye wengine atabarikiwa. Jirani zetu Kenya wanatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu Agosti 8, mwaka huu, nina shauku kuona nao wakiwa na amani kama tuliyonayo Tanzania.

Haimaanishi kuwa wavuruga amani hawapo, la hasha! Kila penye wapenda amani na penye watu wanaosimama kuomba kwa ajili ya amani ya Tanzania, wanaoichukia na kutaka ipotee huibuka.

Lakini, je, tunaweza kujigamba kwamba ni kwa akili na maarifa yetu pekee amani hiyo imeendelea kudumu nchini? Jibu ni hapana, kwa asilimia kubwa ni naamini kuwa ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu anayeangalia na kuifurahia bidii yetu ya kuomba amani.

Nimeona Wakristo na Waislamu nchini, wakiomba kwa bidii kuhusu amani ya nchi yetu na viongozi wake na pia nimeona na kusoma katika vyombo vya habari vya nje ya Tanzania jinsi Wakenya wanavyoomba Mungu awajalie amani katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge unaotarajiwa ndani ya siku chache zijazo.

Kama alivyowahi kueleza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati wa mazungumzo yake na wanahabari Dar es Salaam kuhusu hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ndivyo Watanzania tunavyopaswa kufanya kwaajili ya Kenya.

Balozi Mahiga aliwaomba Watanzania waiombee Congo ili iwe na amani. Alisema jirani zetu wanapokuwa na mapigano, nasi tunakuwa katika wakati mgumu na wa hofu, tukijiuliza itakuwaje machafuko yao yakiendelea?

Kwa mtazamo wa haraka haraka, hata biashara zetu na jirani zetu wenye matatizo, zinakuwa za wasiwasi na hata wakimbizi nao wanakuwa na uwezekano wa kuongezeka ndani ya nchi yetu.

Kwa sababu hizo na za kiusalama, Watanzania tukiwa jicho la amani duniani, tunapaswa kuhakikisha hayo hayatokei kwa kutumia maarifa aliyotupa Mungu (utatuzi wa kidiplomasia), pamoja na kumwomba Mungu awaepushie vurugu. Hakuna linaloshindikana kwa Mungu.