Hatua ya Polisi kukamata wapigadebe iungwe mkono

HIVI karibuni Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilifanya operesheni katika vituo mbalimbali vya daladala na kufanikiwa kuwakamata wapigadebe 150 kwa makosa ya kubughudhi abiria, ikiwa ni pamoja na kuwaibia mali zao.

Jeshi hilo limefanya kazi nzuri kwa kuwa watu hao walikuwa ni kero kubwa kwa wananchi waliokuwa wakitumia vituo hivyo. Watu hao waligeuza vituo kuwa sehemu yao ya kuvutia bangi kiasi kwamba abiria wanaotumia vituo kukosa uhuru na pengine kudhuriwa au kuibiwa mali zao.

Wapigadebe hawa wamekuwa ni kero hasa kwa wanawake kwani mara kadhaa wamekuwa wakitumia lugha za kuudhi na kudhalilisha. Operesheni hii ni muhimu kuungwa mkono na madereva na makondakta kwani nao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiwalea.

Baadhi ya makondakta wamekuwa wakilazimishwa na wapigadebe hao kuwapa pesa kama ujira kwa kuita abiria kupanda ndani ya magari yao, jambo hili si la kiungwana kabisa kwani magari yote yameandikwa ni wapi yanakwenda.

Ni muhimu Jeshi la Polisi likatoa onyo pia kwa Umoja wa Madereva na Makondakta kutowaendekeza wapigadebe hawa kwani malipo kidogo wanayoyapata huwafanya kuweka maskani katika vituo vya daladala kwani wanajua kuna pesa ya bure.

Imekuwa ni ngumu kuwanyima fedha kwani huwatishia makondakta kuwaharibia matairi ya magari na kupasua vioo. Je, hawa wapigadebe wana nguvu kiasi gani kulizidi jeshi la polisi?

Pindi daladala inapokuwa imejaa abiria baadhi yao hudandia na kukwapua mizigo ya abiria ambao wamekaa karibu na mlango, kwa kuwa gari linakuwa katika mwendo ni ngumu kudhibiti aina hii ya wizi.

Ni muhimu jeshi la Polisi likajiwekea mikakati madhubuti ili operesheni hii iwe endelevu kama walivyoahidi wakazi wa Dar es Salaam kwani mara kadhaa baadhi ya mipango huishia njiani.

Wapigadebe hawa waligeuza vituo vya daladala kama makazi yao kwani wengine wamekuwa wakifanya uchafuzi wa mazingira na kusababisha hali ya vituo kuwa mbaya. Ni wakati sasa kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa huru wanapokuwa katika vituo vya mabasi wakisubiri usafiri.

Mwito wangu kwa wananchi kuwafichua watu hao wanaokimbilia katika maeneo yao wakati wa msako huo ili kusaidia jeshi la polisi kufanya kazi yao, lengo likiwa ni kuweka jiji katika hali ya usalama. Ushauri wangu kwa jeshi la polisi msiishie tu kwa watu hao bali hata wale wanaoiba mikoba na kupora simu kwa njia ya pikipiki.

Watu hawa wapo sana maeneo ya Posta na wamekuwa wakifanya matukio hayo majira ya asubuhi, hivyo ni vyema operesheni maalumu kwa ajili ya watu hao ifanywe ili kukomesha kabisa matukio ya wizi kwa jiji hili