Sheria ya usalama barabarani irekebishwe isitelekeze watoto

NCHINI Tanzania ajali za barabarani ni miongoni mwa visababishi vikubwa vya vifo kama ilivyo duniani. Takwimu za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania mwaka 2015, watu 3,468 walifariki dunia na wengine 9,383 kujeruhiwa kutokana na ajali hizo zikihusisha magari, pikipiki, baiskeli na waenda kwa miguu kwa kipindi cha mwaka 2015.

Hivi karibuni nilihudhuria mafunzo ya siku tatu kuhusu usalama barabarani, yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) na kufanyika Kibaha, mkoani Pwani.

Katika mafunzo hayo, ilibainika kuwa Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973 Sura ya 168 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002, ikiwa ndiyo sheria mama inayosimamia masuala ya usalama barabarani sambamba na sheria nyingine katika sekta nyingine, imewasahau na kuwatelekeza watoto.

Sambamba na uchunguzi kupitia vyanzo mbalimbali, ilibainika kuwa pamoja na kujitahidi kudhibiti ajali, bado sheria hii ikiachwa ilivyo, Watanzania hususan watoto watazidi kuangamia kupitia ajali kwani haijitoshelezi kiasi cha kuwa na ubavu wa kukabili na kudhibiti ajali au madhara ajali hizi hasa kwa watoto.

Katika Wazo Langu, nitaonesha namna sheria hii ilivyowajali watu wazima, na kuwaacha watoto kana kwamba hawapo, au hawaathiriki na ajali, ilhali watoto ni miongoni mwa kundi linaloathirika zaidi kwa ajali, wakiwamo waenda kwa miguu.

Ninasema hivyo, kwa sababu Kifungu cha 39 (11) kinamtaka dereva na abiria aliyekaa kiti cha mbele, wafunge mkanda wakati wote wa safari. Lakini ama imesahau, au imewatelekeza kwa makusudi watoto, kwa kutotambua matumizi ya mikanda hiyo kwa abiria wengine wanaokaa nyuma wakiwamo watoto ambao mara nyingi hata katika basi za shule na gari nyingine, wanaonekana wakicheza cheza na kuchungulia dirishani wakati gari likiwa safarini.

Huu ni udhaifu na utelekezaji mkubwa wa usalama wa watoto katika vyombo vya usafiri barabarani. Kadhalika, sheria imekuwa bubu, imelala usingizi na kusahau kuwa, katika vyombo vya usafiri barabarani hususan magari, vinahitajika vizuizi kwa ajili ya usalama wa watoto (child restraints).

Sheria imekaa kimya kana kwamba, watoto hawahitaji usalama barabarani ilhali nao wanaangamia. Rejea ajali ya Mei 6, mwaka huu iliyowakumba wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent jijini Arusha katika eneo la Mlima Rhotia wilayani Karatu na kuua wanafunzi 32.

Kama sheria hiyo ingezingatia na kusisitiza umuhimu wa mikanda kwa watoto, miili ya watoto ingekutwa katika viti vyao, badala ya kuwa pamoja huku ikiwa haina majeraha mengi au makubwa, hali inayoonesha hapakuwa na mikanda wala vizuizi.

Hii ni aibu kwa watunga sera kusahau watoto wa uzao na kizazi chao. Kuhusu vizuizi kwa watoto, sheria imekaa kimya. Hata watunga sera nao wamekaa kimya, wamesahau umuhimu wa watoto kuwa salama barabarani. Viwango vya usalama barabarani kimataifa, vinataka gari kuwa na vizuizi kwa ajili ya usalama wa watoto, sera na sheria zetu hazijui kabisa; wala hazioni.