Maendeleo yanahitaji uwajibikaji, uzalendo

UWAJIBIKAJI na uzalendo ni maneno mawili rahisi sana kuyatamka na kuyaandika. Ni rahisi kwa vile yamezoeleka masikioni na machoni pa walio wengi. Lakini, katika uhalisia na matumizi yake, yamekuwa ni moja ya misamiati ambayo haipendwi hapa nchini.

Kila mmoja katika nafasi yake akiwajibika, nini kinaweza kukwamisha maendeleo? Na tena, uzalendo ukitangulizwa mbele katika kila jambo, hivi fisadi, rushwa, upendeleo, ufujaji mali za umma, ubinafsi, ukabila na udini vitatoka wapi?

Kweli tunahitaji mahakama ya ufisadi kwani wateja wako wa kutosha! Ni ukweli unaouma kwamba Watanzania wamechoka porojo. Wamechoka siasa, sasa wanahitaji vitendo. Ndio maana kama kuna Mtanzania ambaye anataka kufifisha juhudi za Rais John Magufuli akihamasisha watu wasifanye kazi, tena wagomee hata waajiri wao, atapingwa kila kona wakiwemo aliowashawishi.

Hakuna maendeleo yanayoweza kuja bila kuchapa kazi, tena kwa juhudi na maarifa na sio porojo za siasa. Sipingi siasa, bali inakera inapoingizwa siasa kwenye kazi. Tanzania ni ya wote, wanasiasa, wakulima, wafugaji, wavuvi, wanataaluma mbalimbali wakiwemo wanasheria, madaktari na wengineo. Tunahitaji kutumia ujuzi wetu bila kusubiri jirani kutoka nje ya nchi kutuletea maendeleo.

Wapo wataalamu wa kada mbalimbali, lakini wanahitaji kuwa na uzalendo ili kuiwezesha nchi hii kufikia lengo la kuwa nchi ya viwanda. Wakulima wana nafasi yao kubwa. Wakilima kwa malengo, watatoa malighafi ya viwanda. Tuna nchi kubwa yenye rutuba.

Tunahitaji teknolojia kidogo kutumia mito na maziwa tulivyojaliwa na Mungu katika kilimo chetu badala ya kusubiri mvua za msimu. Tunahitaji kuelewa mazao yanayovumilia ukame na pia kuelewa aina ya udongo na aina ya mazao yanayohitajika.

Wataalamu wa kilimo wakijipanga, hakuna haja watu kuendelea kumiminika mjini. Utajiri uko mashambani ilimradi tulime kwa kufuata utalaamu. Wasomi watumie ujuzi kuwekeza teknolojia katika uzalishaji. Wanasheria watetee wanaodhulumiwa badala ya kuwa wanasiasa. Walimu wafundishe vijana wetu ili tuwe na taifa la wasomi badala ya kukalia migomo na madai yanayoshughulikiwa tayari.

Waandishi waandike habari za kuchochea maendeleo badala ya kuandika habari za uchochezi na uhasama katika jamii. Wakurugenzi wa halmashauri nao wawajibike. Wakuu wa mikoa na wilaya wasimamie mipango ya serikali kumpunguzia Rais Magufuli adha ya kusimamishwa njiani kwa kuwa wananchi hawana mahali pa kupeleka kero zao. Kumbe hata watendaji wa serikali za mitaa nao wafanye kazi zao Hii ikifanyika, nchi itakuwa imepata mwarobaini!