Mawakala fuateni utaratibu muwaepushie usumbufu mabondia

JANA ilitoka taarifa katika vyombo vya habari habari ikizungumzia kuzuiliwa kwa mabondia wawili wa ngumi za kulipwa, Francis Miyeyusho na Salehe Mkalekwa kwenda nchini Hungary.

Wawili hao walizuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, ilikuwa waelekee nchini humo kwa ajili ya mpambano wao uliokuwa ufanyike jana. Kuzuiliwa huko kunatokana na Kamisheni ya Ndondi za Kulipwa (TPBC) yenye dhamana ya kusimamia ndondi hizo kuweka zuio ya safari hiyo.

Hatua hiyo ya TPBC inatokana na ukweli kuwa mawakala wa mabondia hao hawakuwa na kibali kutokea TPBC na wala Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.

Binafsi ningependa kuchukua wasaha huu kuwasihi mawakala wa mabondia wa hapa nchini kuzingatia weledi katika ufanyaji wa kazi zao. Haiingii akilini kwa mawakala kuingia mkataba na mabondia pamoja na mapromota wa ngumi wa nchini Hungary bila ya kwanza kuwa na kibali kutokea TPBC ilihali wanajua fi ka kuwa ni kinyume na taratibu.

Sasa kwa mchezo ambao ilikuwa ufanyike leo nchini humo inakuwaje wakati mabondia ndiyo kwanza wamezuiliwa hapa nchini ni nani ambaye atalipia gharama zinazokuwa zimepatikana.

Ni wazi kuwa kinachotakiwa kikubwa ni weledi na uzingatiwaji wa taratibu husika katika michezo, hii siyo tu kwa mabondia ila ni kwa wanamichezo na wasanii wote kuhakikisha kuwa wana vibali vya kazi wanazoenda kufanya.

Lakini pia mawakala hawa wanakuwa wamewaathiri mabondia wenyewe ambao walikuwa waelekee nchini humo kimchezo na kwa kuzuiliwa huko wanaathriwa kisaikolojia. Ili kuondokana na hali hiyo ambayo inarejesha nyuma thamani ya mchezo ni vema basi kwa wahusika wenyewe kuhakikisha kuwa wanazingatia taratibu ili wasijiharibie uaminifu hata kwa mapromota hao wa nje ambao wanashirikiana nao kimichezo.

Nisingependa kuona hilo linaendelea kujitokeza tena kwa kuwa kwa kufanya hivyo kunasababisha ule mtazamo wa kuwa bondia ni wanamichezo wahuni na watu ambao ni wababaishaji.

Ni dhahiri kuwa kwa kuzuiliwa kusafi ri tena wakiwa Uwanja wa Ndege siyo tu wamejidhalilisha wao ila ikumbukwe kuwa wameiaibisha tasnia hiyo ambayo iliwahi kuhusishwa na usafi rishaji wa dawa za kulevya.