Baada ya KDA kuvunjwa, Kigamboni sasa mjipange

RAIS John Magufuli wiki iliyopita alitangaza kuivunja Mamlaka ya Usimamizi wa Mji Mdogo wa Kigamboni (KDA) na sasa kuhamishia shughuli zake katika Manispaa ya Kigamboni.

Kuvunjwa kwa KDA kunatokana na mgongano wa muda mrefu katika usimamizi wa ardhi kati ya KDA na Manispaa ya Kigamboni ambao walijikuta wakitakiwa kufanya kazi moja, hivyo Rais aliamua kuivunja mamlaka hiyo na kuiachia Manispaa ya Kigamboni kuendelea na kazi zilizokuwa zikifanywa na KDA.

Jukumu la KDA lilikuwa kusimamia, kupima na upangaji wa mji wa Kigamboni wakati jukumu hilo pia ni la manispaa hiyo, hivyo mgongano huo wa usimamizi wa ardhi Kigamboni ulisababisha migogoro mingi ya ardhi tangu ilipozaliwa Manispaa ya Kigamboni mwaka 2015.

Kwanza uamuzi huo wa Rais pamoja na kupongezwa na hasa wakazi wa Kigamboni ambao walisimamisha shughuli zao katika uendelezaji wa ardhi, lakini pia utatoa fursa kwa watu wengi kuwekeza katika ardhi ya Kigamboni na hivyo mji huo kutanuka zaidi.

Ni vizuri, wakati tukisherehekea sasa kuisha kwa migogoro iliyokuwa ikisababishwa na mwingiliano wa kazi kati ya KDA na Manispaa ya Kigamboni, viongozi wa mji huo kujipanga kusimamia vizuri upangaji wa wake.

Kigamboni bado ni mji mpya hivyo ni rahisi kuupanga vizuri na ukapendeza tofauti na manispaa nyingine ambazo tayari zimeshaharibika kwa ujenzi holela. Rais amepokea maombi ya kuivunja KDA kutoka kwa Wanakigamboni, Wanakigamboni kwa kushirikiana na viongozi wa Manispaa hiyo tumsaidie Rais kuupanga mji wa Kigamboni upendeze.

Manispaa ya Kigamboni izingatie maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyoyatoa wakati akitangaza uamuzi huo wa Rais wa kuivunja KDA, ambapo aliwataka madiwani na watendaji wa Kigamboni kuhakikisha sasa wanasimamia mipango miji ya mji huo.

Naamini sasa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, Stephen Katemba kwa kushirikiana na watu wake wa chini watakuwa macho kuhakikisha kwamba vile vikwazo vyote vinaondoka kwa watu kupimiwa na kupata vibali vya ujenzi mapema ili kuhamasisha watu kujenga maeneo yaliyopimwa na kupangwa.

Naamini pia kuwa kama manispaa hiyo itakuwa macho hakuna mtu ambaye atajenga eneo ambalo hakutakiwi kujengwa kama vile kuzuia barabara za mitaa pamoja na njia za miundombinu mingine jambo ambalo husababisha hatari baadaye.