Matundu Sheria Usalama Barabarani yazibwe

NCHINI Tanzania, suala la usalama barabarani husimamiwa na Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 1973, Sura ya 168 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002.

Kwa kiasi kikubwa, sheria hii inafanya vizuri kukabili tatizo la ajali barabarani zinazozidi kuliangamiza taifa kwa kusababisha vifo, majeruhi au ulemavu kwa watu. Mratibu wa Mradi wa Usalama Barabarani wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Gladness Munuo anasema: “Ajali zinaondoa nguvu kazi ya taifa, zinagharimu mamilioni ya pesa kutibu waathirika na hasa kusababisha umasikini katika familia jambo ambalo kwa kiasi kikubwa, linawaathiri wanawake.”

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dk Boniphace Respicious wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na wenzake Aprili- Septemba 2014 katika hospitali sita za umma kuhusu majeruhi waliotokana na ajali, kati ya majeruhi 4,675, asilimia 76.6 walikuwa wanaume huku asilimia 70.2 wakiwa kati ya miaka 18 na 45 ambayo ndiyo nguvu kazi.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Wadau kutoka Asasi za Kiraia unaotetea Marekebisho ya Sheria na Sera ihusuyo Usalama Barabarani Tanzania, sheria hiyo bado ina upungufu unaohitaji marekebisho makubwa.

Wabunge na watunga sera wetu wajue kuwa, sheria hii ina ‘matundu’ yaani upungufu mkubwa unaostahili ‘kuzibwa’ yaani suala la mwendokasi; uvaaji wa mikanda kwa abiria; uvaaji wa kofia ngumu kwa wapanda pikipiki; ulevi au unywaji pombe, pamoja na suala la vizuizi kwa watoto.

Katika Kifungu cha 44, Sheria inakataza mtu kuendesha akiwa amekunywa pombe zaidi ya kipimo kilichowekwa kisheria kijulikanacho kama Grams Per Decilitre (g/dL) ambapo hapa Tanzania ni 0.08 g/dl.

Kiwango cha kilevi kilichotamkwa na sheria hii ni kikubwa ukilinganisha na tafiti zilizofanyika na kupendekezwa, pamoja na kiwango kinachokubalika kimataifa. Munuo anasema: “Sheria irekebishwe ili iendane na kiwango cha kimataifa ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na 0.02g/dl kwa dereva asiye mzoefu.”

Hapa, sheria inapaswa kutamka wazi maana ya dereva mzoefu na ieleze asiye mzoefu ni yupi. Kuhusu vizuizi kwa watoto, sheria ni ‘bubu’. Haizungumzi chochote kuhusu vizuizi kwa watoto kama ilivyo mikanda kwa abiria wakubwa wawapo katika gari.

Ukimya huu unaonesha sheria imetoboka maana iko kinyume na viwango vya usalama barabarani kimataifa kama kwamba haiwajui wala kuwajali watoto. Kwa kuwa watoto nao wanaathirika na ajali, sheria irekebishwe ili iagize magari kuwa na vizuizi kwa watoto.