Vyama vianze sasa maandalizi Madola

MICHEZO ya 21 ya Jumuiya ya Madola itafanyika Gold Coast kuanzia Aprili 4 hadi 15 mwakani na Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotarajia kupeleka timu.

Nchi nyingine tayari zimeanza maandalizi ya kushiriki michezo hiyo ili kuhakikisha zinafanya vizuri katika michezo hiyo. Tanzania inatarajia kupeleka timu za riadha, kuogelea na ngumi, lakini hatua hiyo itafanyika endapo timu hizo zitafi kia vigezo vinavyokubalika.

Hadi sasa, wanariadha wanane pekee ndiyo wenye uhakika wa kushiriki michezo hiyo kwani ndiyo waliofi kia viwango baada ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia ya riadha London, Uingereza.

Kuogelea nao wameshiriki mashindano mengi, lakini tatizo liko kwa timu ya ndondi licha ya sasa kuwepo katika mazoezi makali ya kujiandaa na michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola. Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) limeshindwa kabisa kuipeleka timu zake za taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kutokana na ukosefu wa fedha.

BFT tangu waingie madarakani miaka minne iliyopita, wameshindwa kupeleka timu ya taifa katika mashindano ya dunia au yale ya Afrika na hivyo, kuwa na nafasi fi nyu ya kufuzu kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Viongozi wa BFT wameshindwa kabisa kusaka fedha kwa ajili ya maendeleo ya mchezo huo hapa nchini na kuzifanya ndondi kuporomoka kila kukicha. Chama cha Kuogelea (TSA) chenyewe kimekuwa kikijitahidi kuwapeleka wachezaji wake katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ili kuwapa angalau uzoefu wa kimataifa, kitu ambacho ni kizuri na mfano bora.

Sijui wenzetu wa BFT wameteleza wapi kwani miaka ya nyuma mchezo huo ulitamba hadi kuiwezesha Tanzania kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Kuala Limpur, Malaysia 1998.

Bondia Michael Yomba Yomba (sasa marehemu) ndiye aliyeitoa Tanzania kimasomaso katika mchezo wa ndondi baada ya kutwaa medali hiyo ya dhahabu. Mbali na Yomba Yomba, mabondia wengine waliowahi kutamba ni Titus Simba, Rashid Matumla, Haji Matumla, Hassan Matumla, Mbwana Matumla, Mzonge Hassan, Koba Kimanga na wengine, ambao walifanya vizuri kimataifa.

Aprili siyo mbali, hivyo vyama au mashirikisho ya michezo wajitahidi kuwaandaa vizuri wachezaji wao ili kwanza wafi kie viwango na pili waweze kufanya vizuri katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola.