Trafiki ongezeni mbinu kuzikabili ajali barabarani

LICHA ya jithada zinazofanywa na wadau mbalimbali wa usalama barabarani kukabiliana na ajali, bado zinatokea kila kukicha huku nyingine zikisababishwa na uzembe wa madereva na watumiaji wengine wa barabara.

Mfano ni ajali iliyotokea juzi na kusababisha vifo vya watu 15 huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya gari la mizigo aina ya Fuso lenye namba za usajili T425 BFF walilokuwa wakisafiria kugonga mwamba na kupinduka.

Abiria hao walikuwa wakitoka mjini Sumbawanga kuelekea Kijiji cha Wampembe katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, Rukwa. Hiyo ni moja kati ya ajali zilizopoteza maisha ya watu wengi kwa mwaka huu na kibaya zaidi, ni ajali iliyochangiwa na uzembe wa dereva, na hata abiria.

Kwanza ninawapa pole wafiwa na wale majeruhi nawatakia heri wapone haraka, lakini bado ninasisitiza kuwa ni uzembe wa abiria na dereva kwa sababu Fuso hilo lilikuwa limebeba mizigo huku pia abiria nao wakipanda humo humo, kitu ambacho ni hatari zaidi dhidi ya usalama barabarani.

Dereva alifahamu ubaya wa kusafirisha abiria na mizigo kwa pamoja, hivyo hakupaswa kuwasafirisha hivyo, kadhalika, abiria nao hawakupaswa kukubali kusafirishwa hivyo. Taarifa ya Polisi mkoani Rukwa inasema gari hilo lilikuwa katika mwendo wa kasi huku ikisemekana kuwa dereva hakuwa akifahamu vizuri maeneo wanayoyapita.

Kimsingi, jamii haiwezi kukaa kimya na kusema “ajali ni ajali,” bila kuchukua hatua madhubuti kuzikataa ajali hizo, ikiwa ni pamoja na abiria kutoa taarifa sahihi kuhusu madereva wanaokikuka kanuni za usalama barabarani ukiwamo mwendo wa kasi kupita kiasi na ujazaji mizigo na abiria usio rafiki wa usalama.

Licha ya idadi ya askari nchini kutokuwa ya kutosha, askari wa usalama barabarani wanapaswa kudhibiti maeneo ya upakiaji abiria na mizigo, na kuweka mitego kubaini ukiukwaji unaofanywa na kuchukua hatua za kisheria.

Katika maeneo ya namna hiyo, lengo lisiwe tu kukamata na kuwatoza faini madereva wazembe, bali pia kuonya na kutoa elimu endelevu kwa madereva na watumiaji. Yapo maeneo kadhaa nchini ambapo elimu mintarafu usalama barabarani ni adimu.

Hata hivyo, Jeshi la polisi kwa siku za hivi karibuni limejitahidi kufanya kazi nzuri ingawa, kazi hiyo inapaswa kuendelezwa na kuimarishwa ili yaonekane matunda chanya katika vita dhidi ya ajali. Ubunifu wa mbinu mbalimbali katika vita hii unahitajika.

Abiria nao watambue wajibu wao katika vita hii, badala ya kushiriki kusababisha ajali, kisha wakaanza kulalamika madhara yanapotokea. Tunataka ajali zisitokee, lakini zikitokea, madhara yawe kidogo. Ulevi na mwendokasi ni vyanzo vikubwa; vipigwe vita