Watumishi wa Umma, msikieni Mkuchika

WIKI iliyopita Waziri wa Nchi Ofi si ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika wakati akikabidhiwa ofi si na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Angela Kairuki alitoa mwito kuwataka watumishi wa umma kuacha kutumia muda mwingi kunywa chai na kujikuta wakichelewa kuwahudumia wananchi.

Katika kuhakikisha kuwa agizo lake hilo linatekelezwa alizishauri Ofisi za Umma nchini kufungua migahawa katika maeneo ya Ofisi zao na kama ikitokea wakishindwa wao kuiendeleza basi watangaze zabuni ili wapatikane watakaoiendesha, lengo kubwa likiwa ni kuwawezesha wafanyakazi kupata huduma hiyo kwa ukaribu.

Binafsi ninaunga mkono hoja hiyo ya Waziri Mkuchika kwa kuwa wapo watumishi wa umma ambao hutumia muda mwingi kupata kifungua kinywa asubuhi ambapo huunganisha na upigaji wa soga, hivyo kutumia muda mwingi zaidi wakati wananchi wakisubiria huduma.

Hii imekuwa na athari kubwa zaidi hasa kwa wananchi wanaotokea mikoani kwa kuwa hujikuta wakilazimika kulala maeneo ya mijini ambapo wanakuwa wameenda kufuata huduma hiyo na kuchelewa kuipata au kutoipata kabisa kwa muda stahiki.

Nisingependa kuishia tu kwenye unywaji wa chai kuwa ni sababu kubwa ya uzorotaji wa huduma za kiofisi ila yapo mengine mengi zaidi. Wapo watumishi wa umma ambao dhana ya Hapa Kazi tu ni kama haiwahusu kwa kuwa bado wanapenda kufanya kazi kimazoea huku wito wa kuhudumia wananchi ukiwa umepungua.

Utakuta wanatoa majibu yasiyostahili kwa watu ambao wanakwenda kupata huduma kwenye ofisi zao, hii imesababisha kuzorotesha maendeleo katika sekta husika. Ni vema watumishi hao wakatambua kuwa ni jukumu lao kuwahudumia wananchi na siyo hisani na hasa ikizingatiwa kuwa kazi wanayoifanya ni kazi ya serikali.

Kinachotakiwa ni juhudi za kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kufanya kazi kwa nia na upendo ili kuendelea kusaidia malengo ya serikali kuwafikishia wananchi wake huduma bora yanafanikiwa.

Ni vema kwa wakuu wa Idara mbalimbali serikalini wakabuni njia mbadala itakayowabaini watendaji wazembe na hasa wale ambao kama alivyowataja Waziri kuwa wanatumia muda mwingi katika chai au chakula cha mchana badala ya kufanya kazi.