Afrika Mashariki ishirikiane kulinda utu wa mtoto wa kike

HIVI karibuni dunia iliadhimisha siku ya mtoto wa kike, ambapo viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo wa Afrika Mashariki, walishiriki katika maeneo yao, kuhakikisha wanaweka mipango na mikakati, itakayohakikisha mtoto wa kike analindwa pamoja na kuondolewa vikwazo katika kutimiza malengo yake.

Vipo vikwazo mbalimbali anavyokumbana navyo mtoto wa kike katika kufikia malengo yake ya kimaisha, ikiwemo ukeketaji, ndoa za umri mdogo na hata mimba za utotoni, ambavyo kwa namna moja hadi nyingine vinaweza kusababisha asiweze kufikia malengo yake.

Ikumbukwe kuwa nchi za Afrika Mashariki, zinapakana katika baadhi ya mikoa huku wananchi waishio katika maeneo hayo, wakiwa na muingiliano wa karibu katika masuala mbalimbali.

Ili kuona umuhimu wa mtoto wa kike, nchi za Afrika Mashariki ziliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo pamoja na kutoa matamko mbalimbali, yenye kuhitaji ufuatiliaji na usimamizi ili mtoto wa kike aweze kuwa salama wakati wote.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Tanzania ilizindua kampeni itakayohusisha mikoa 10 kwa ajili ya kulinda, kuwapenda, kuthamini na kuwezesha mtoto wa kike kufikia malengo yake kwa kuondolewa vikwazo vyovyote anavyokumbana navyo, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ukatili, kupata mimba katika umri mdogo na hata ndoa za utotoni.

Licha ya kuwepo kwa vikwazo vya aina mbalimbali vinavyosababisha mtoto wa kike kutofikia malengo yake, lakini ukatili ni aina mojawapo inayoendelea kusababisha mtoto wa kike kutofikia ndoto zake katika maeneo mbalimbali.

Katika maadhimisho hayo, kila nchi ilikuwa na azma moja ya kuhakikisha inasimamia na kuhakikisha utu wa mtoto wa kike unalindwa, kwa kuwa yapo makundi mbalimbali ya wasichana walioshindwa kufikia malengo yao kutokana na kufanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili.

Kwa maadhimisho hayo, kila nchi ilisimama na kuungana kwa kutoa matamko mbalimbali yenye kuonesha wazi ni kwa jinsi gani usimamizi dhidi ya mtoto wa kike unahitaji kupewa kipaumbele, ili kujenga jamii yenye haki na usawa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa mfano kupitia mitandao mbalimbali, viongozi wa serikali ya Kenya na mashirika mbalimbali ya kijamii kwa pamoja walitangaza mwito wa umuhimu wa haki za mtoto wa kike, ikiwemo kupata elimu, kuzuia ndoa za utotoni na mapambano dhidi ya ubakaji.

Aidha, serikali hiyo iliahidi kutoa Sh bilioni 9 zitakazotumika kwa ajili ya maendeleo ya watoto yatima na wasichana wasiojiweza nchini Kenya, lakini pia kuchukuliwa kwa hatua kali watakaopatikana na hatia ya kukiuka haki za watoto wa kike.

Kauli hiyo ilitolewa na viongozi wa Kenya, kwa kutambua ni kwa jinsi gani mtoto wa kike anahitajika kuheshimiwa na kuthaminiwa, akiondolewa vikwazo vyovyote ili kujenga jamii yenye usawa na haki ingawaje nchi nyingine nazo zilitoa matamko mbalimbali.