Tusiwabeze wanaohama vyama; ni haki yao

VYOMBO vya habari juzi na jana vilitawaliwa na habari za wanasiasa sita kutoka vyama vya upinzani, kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kupokelewa rasmi na Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Wanachama waliojiunga na CCM ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha aliyehamia Chadema katika harakati za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Protabas Katambi.

Wengine waliojiunga na CCM walikuwa wanachama wa ACT-Wazalendo akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba, Edna Sungu na Wakili wa Kujitegemea wa chama hicho, Albert Msando.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, naye amerejeshwa CCM baada ya awali kuvuliwa uanachama kwa madai ya kukisaliti chama katikauchaguzi mkuu uliopita.

Ikiwa ni miaka miwili ya Rais John Magufuli katika utawala wake, wanachama hao wamejiunga na CCM kwa kuwa wamekubali jitihada na kazi mbalimbali anazozifanya. Jitihada hizo ni pamoja na kuwajali wananchi wa hali za chini, kuwaondoa wafanyakazi hewa na wale wenye vyeti feki, kusimamia na kupiga vita rushwa na ufisadi na kuamsha amri ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma huku akisimamia kwa dhati rasilimali za umma yakiwamo madini. Hatua za kurudi kwa wanachama hao ni ishara ya wazi kuwa wamevutiwa na utendaji kazi wake ambao umebadilisha taswira ya chama hicho.

Si vibaya kwa mtu kutoka chama kimoja kwenda kingine kwa mapenzi yake mwenyewe kwa kuwa siasa siyo uadui na mtu anayo haki na uhuru wa kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine.

Hata hivyo, maamuzi yaliyofanywa na viongozi hao, kumezua mijadala mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuwa huenda watu hao wamekumbwa na ‘njaa’, yaani hali mbaya ya kiuchumi hivyo, kujiunga na chama tawala hicho ili kupata unafuu wa maisha.

Sipingani na uhuru wa maoni wa watu, lakini pia siungi mkono mambo ya kuwabeza waliofanya maamuzi yao kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inatoa uhuru wa mtu kufanya chochote mradi tu, havunji sheria.

Kuwakejeli waliofanya maamuzi yao, bila kuvunja katiba wala sheria za nchi, ni kutowatendea haki watu hao waliovutwa na utendaji uliotukuka wa Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Magufuli.

Ndiyo maana ninasema, “Hongera Rais John Magufuli kwa kuirudisha Tanzania kwenye mstari.” Hongera waliofanya maamuzi yao kurudi chama tawala, bila kushinikizwa na lolote kwa kuwa wametumia haki yao ya kidemokrasia