Nchi za EAC zikabili ajali za barabarani

AJALI za barabarani ni moja kati ya majanga yanayopoteza maisha ya watu kwa nchi za Afrika Mashariki huku wengine wakibaki kuwa na ulemavu wa kudumu.

Hali hiyo imechangia kupungua kwa nguvu kazi ya mataifa ya Afrika Mashariki. Ajali hizi zimekuwa zikitokea kwa njia mbalimbali, zipo zinazosababishwa na uzembe wa madereva, uchakavu wa miundombinu, uchakavu wa vyombo vya usafiri na mengineo mengi.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka jana uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) wastani watu watatu kati ya kila watu 10,000 hupoteza maisha katika nchi za Afrika Mashariki, kila siku.

Kwa nchi hizo, Tanzania ndiyo inaongoza kuwa na idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na ajali. Takwimu zinaonesha kuwa, waliokufa mwaka jana ni 3381 ikifuatiwa na Uganda iliyopoteza watu 3300, kisha Rwanda, Kenya, Burundi zikifuata.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani hapa nchini, Fortunatus Muslim, ajali zimepungua kufikia asilimia 42 kati ya mwaka 2016 na mwaka 2017. Tanzania na Kenya ni nchi zinazotekeleza mradi wa Bloomberg unaoshirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoyataja mambo matano muhimu yanayosaidia kupunguza ajali za barabani.

Maeneo hayo ni ufungaji wa mikanda, matumizi ya kofia ngumu kwa waendeshaji wa pikipikipi, kuzuia unywaji wa pombe, matumizi ya viti maalumu kwa watoto, mwendo kasi uliopitiliza.

Kwa haja ya kupangwa upya kwa mikakati itakayosaidia kuondoa ajali hizi za barabarani na hasa ni kwa njia ya kuimarisha Sheria za Barabarani, kutoa elimu kwa watumiaji wa vyombo vya moto pamoja na kuwapo kwa nia ya dhati ya kuzibadili sheria za usalama wa barabarani zilizopitwa na wakati.

Iwapo hayo yakifanyika ni imani yangu kuwa ajali zitapungua kwa kasi na kuepusha kupoteza nguvu kazi ya taifa inayopotea kila mwaka kufuatia ajali hizo za barabani. Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa usalama wa barabarani zishirikiane na wadau wengine katika kuendeleza elimu za usalama wa barabarani kwa wananchi ili nao washiriki katika kukabiliana na ajali hizo.

Kwa kuwa kwa hapa nchini tayari mchakato wa kuzibadilisha sheria za usalama wa barabarani zilizopitwa na wakati ulishaanza ni vema ukamalizika kwa haraka ukapelekwa muswada bungeni ili upitishwe na kisha kusainiwa na Rais John Magufuli ili sheria mpya zianze kushugulikia makosa hayo ya usalama barabarani.

Mwaka 2018 nchi za Afrika Mashariki ziungane kupiga vita ajali hizo ili Ukanda wa Afrika Mashariki uepuke ajali. Wakuu wa vikosi vya usalama wa barabarani wa nchi hizo wajadiliane namna ya kuondoka kero za ajali katika nchi zao huku wanahabari wakiendelea kutoa msisitizo wa mabadiliko ya sheria ili ziwepo zinazoweza kukabiliana na changamoto zilizopo.