Ni muhimu kwa wabunge EALA kudumisha mshikamano

WABUNGE wateule wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wanaowakilisha nchi zao ndani ya jumuiya hiyo, hatimaye jana waliapishwa ili kuanza majukumu yao kuiwakilisha jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kuapishwa kwa wabunge wa jumuiya hiyo hapo jana, kuna maana kuwa wabunge wote kutoka nchi wanachama wa EAC, watakuwa na jukumu moja la kuhakikisha wanatoa hoja zenye lengo moja la kujenga mshikamano wa jumuiya hiyo na kutatua changamoto zote zinazoikabili jumuiya kwa uzito wake.

Katika bunge hilo la EALA ,Tanzania inawakilishwa na wabunge Josephine Lemoyan, Happiness Lugiko, Pamela Maassay, Dk Ngwaru Maghembe, Dk Abdullah Makame, Habib Mnyaa, Fancy Nkuhi, Maryam Ussi na Adam Kimbisa aliyerejea tena katika bunge hilo baada ya kipindi fulani kupita.

Bunge hilo lenye lenye makao yake makuu jijini Arusha, awali lilitarajiwa kuanza vikao vyake tangu Juni 4, mwaka huu na kumalizika Juni 5, mwaka huu, lakini ilishindana baada ya nchi tatu tu za Uganda, Tanzania na Burundi, kukamilisha taratibu zote huku Sudan ambaye ni mwanachama mpya wa EALA, ikishindwa kuwasilisha wajumbe wake baada ya kujitokeza kwa dosari ya uchaguzi ili kuwapata wawakilishi wake.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Bunge hilo, Bobi Odiko, wabunge wa EALA jana walitarajiwa kufanya uchaguzi wake ili kumpata Spika wa Bunge hilo katika kikao kilichoanza hapo jana, kikitanguliwa na shughuli nzima ya uapishaji wa wabunge wote.

Ibara ya 49 ya mkataba wa EAC inataja majukumu ya Bunge la EALA kuwa ni kushirikiana na mabunge ya nchi wanachama katika mambo yanayohusu jumuiya, kujadili na kuthibitisha Bajeti ya Jumuiya.

Majukumu mengine ni kupitia na kujadili ripoti mbalimbali zinazohusu jumuiya, kujadili taarifa za hesabu zilizokaguliwa na mambo yote ya msingi ya jumuiya na kutoa mapendekezo kwa Baraza la Mawaziri, kadiri itakavyoonekana inafaa, kulingana na mkataba wa EAC.

Pamoja na hayo, pia Bunge hilo limepewa mamlaka ya kuunda kamati mbalimbali kadiri itakavyoonekana inafaa, ambapo moja ya majukumu ya kamati hizo ni kufanya kazi ya uangalizi wa utekelezaji wa mkataba ulioanzisha EAC na utekelezaji wa mkakati wa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hasa katika maeneo yanayohusu ushirikiano wa jumuiya na kutekeleza majukumu mengi ya Bunge.

Pamoja na shughuli hizo, kazi kubwa ya Bunge hilo ni kutunga sheria, kupitisha miswada mbalimbali, kufanya kazi ya usimamizi au uangalizi wa mihimili mingine ya EAC na kuwawakilisha wananchi wa eneo la jumuiya ili kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na mtangamano wa kisiasa.

Kimsingi kila mwakilishi ndani ya bunge hilo la Afrika Mashariki, anapaswa kuwajibika kikamilifu kama mwakilishi kwa wananchi na Taifa analoliwakilisha, hivyo ni vyema katika kipindi chote anacholiwakilisha bunge hilo, akazingatia sheria na taratibu zinazolisimamia bunge hilo, badala ya kuwa chanzo cha utengano ndani ya bunge hilo.

Nasema hilo kwa kuwa tumeshashuhudia katika baadhi ya mabunge, wawakilishi wakishindwa kuwa kitu kimoja na kujikuta wakishindwa kuyawakilisha vyema mabunge yao pamoja au ajenda za nchi wanazoziwakilisha.

Naamini kuwa kitendo wawakilishi wote kuwa pamoja ndani ya bunge hilo, kutasaidia kuboresha mshikamano wa nchi wanachama na hivyo kuziwezesha kupiga hatua kubwa za kimandeleo.