Elimu inahitajika kuondoa udumavu

KATIKA gazeti hili toleo la jana, kulikuwa na makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Rukwa chakula tele, udumavu juu’.

Makala hayo yalieleza kuwa Utafiti wa Kidemografia na Hali ya Huduma ya Afya mkoani Rukwa (TDHS) wa mwaka 2015- 2016, unaonesha kuwa asilimia 56.3 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, walionekana kuwa na udumavu wa mwili na akili.

Utafiti huo ulionesha pia kuwa asilimia 52 ya watoto wote wa mkoa huo, walikuwa na upungufu wa damu. Hali hii ni hatari kwa ustawi wa mtoto na pia maendeleo kwa ujumla ya afya ya watu wa mkoa huo.

Tatizo la mkoa wa Rukwa liko pia katika mikoa mingine hapa nchini pamoja na nchi nyingine za Afrika, ambako pamoja na kwamba uzalishaji wao wa mazao ya chakula ni mkubwa, lakini kuna tatizo la udumavu kwa asilimia kubwa ya watoto.

Hata hivyo, mbinu pekee ya kuondokana na hali hii ni kutenga kiwango cha fedha ili kukabiliana na tatizo hilo katika miradi ya afya, kilimo na elimu kwa umma. Kupitia miradi hiyo, nchi husika zikizingatia kutenga bajeti katika suala la lishe, zitaweza kupambana na utapiamlo pamoja na udumavu.

Kulingana na tafiti zilizofanyika kwa miaka tofauti, katika nchi za Afrika Mashariki, ni nchi mbili tu ambazo zilifanikiwa kutenga bajeti kubwa ya lishe, ambayo kwa kiasi fulani ingesaidia.

Tanzania ilitenga asilimia 4, Ethiopia walikuwa na asilimia 67, Burundi asilimia 5, Rwanda asilimia 56, Kenya asilimia 44 na Uganda asilimia 43. Kuna mikoa ambayo licha ya kuwa na chakula kingi kwa maana ya mazao ya kilimo, pia ina mifugo mingi na pia kuna uvuvi.

Kuzalisha mazao mengi na kuwa na chakula tele ni jambo moja, lakini kuwa na uelewa wa namna ya ulaji na uandaaji wa vyakula, ni jambo jingine, ambalo linahitaji elimu ya kutosha kwa wananchi.

Kwa hiyo, tatizo la wananchi wengi sio chakula, bali ni namna ya kula chakula hicho kwa usahihi, kikiwa na virutubisho vyote muhimu ili kuboresha afya zao. Ni wazi elimu ya lishe, bado inahitajika katika maeneo mengi ili wananchi wawe na uelewa juu ya lishe, waelewe ni vyakula vipi muhimu kwa afya zao, hasa kwa ukuaji wa mtoto.

Pia wanatakiwa kuelewa namna ya kuandaa chakula. Elimu duni kwa wananchi, ndiyo changamoto kubwa ambayo inafanya idadi kubwa ya watoto vijijini kuwa na udumavu. Wananchi hawajui mama akiwa mjamzito, anatakiwa kula nini ili kumpa afya bora yeye mwenyewe na pia kujenga afya ya mtoto aliye tumboni.

Hali kadhalika, mtoto anapozaliwa wakati wa unyonyeshaji mama ale nini na akifikia umri wa kuanza kulala, mtoto apewe vyakula gani. Udumavu kwa mtoto una athari kubwa, sio tu kwa mwili wake, lakini pia akili hasa katika maendeleo yake darasani.

Kwa mujibu wa wataalamu, kikombe kimoja cha maziwa kila siku, kinaweza kunuokoa mtoto na udumavu. Lishe duni katika siku 1,000 za kwanza za mtoto tangu kutungwa mimba kama hazikuzingatiwa, ina athari kubwa kwa mtoto, ambapo anaweza kudumaa kiakili na kuharibu maisha yake yote.

Hivyo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, watoe elimu kwa wananchi, kuhakikisha watoto hawapati tatizo la udumavu.