Nchi za EAC zitekeleze makubaliano yake

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinadumisha ushirikiano wake kadiri ya makubaliano, mikakati ya masuala mbalimbali kuhakikisha zinakua kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kuwaletea maendeleo makubwa watu wake.

Nchi za EAC, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zina ukubwa wa mita za mraba milioni 2.4 na watu milioni 170. Tangu kuanzishwa kwa EAC, uamuzi mbalimbali umefikiwa au uko hatua mbalimbali za majadiliano kwa lengo la kuleta manufaa yakiwemo maendeleo ya wananchi wake.

Moja ya mambo mtambuka kwa nchi za EAC ni suala la kuzuia mifuko ya plastiki ili kulinda na kutunza mazingira, ambalo nchi hizo kwa pamoja zilikubaliana kukabiliana nalo na tayari Rwanda na Kenya zimechukua hatua huku Tanzania, Uganda, Burundi na Sudan Kusini zikiendelea na mchakato wa kupiga marufuku.

Nchi hizo zina makubaliano ya kuondoa nguo za mitumba kulinda viwanda vya ndani.

Jambo hilo limezifanya ziwe na mikakati ya pamoja. Tayari Marekani imetishia kuziwekea vikwazo nchi za EAC endapo zitaanza kutekeleza uamuzi wake wa kuachana rasmi na nguo za mitumba.

Uamuzi wa kupiga marufuku mitumba hiyo ulifanywa Machi mwaka 2016 kwa kupitisha azimio la nchi wanachama kuachana rasmi na uagizaji wa nguo za mitumba ifikapo mwaka kesho kwa lengo la kulinda viwanda vya ndani.

Kama alivyosema Waziri wa Mazingira nchini Kenya, Charles Sunkuli kuwa ushirikiano baina ya nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki unaotakiwa kusaidia kuondoa mifuko ya plastiki unatakiwa kwa masuala mengine pia.

Katika kuondoa bidhaa kama hizo kunaweza kutokea changamoto kwa wazalishaji au wafanyabiashara wanaojipatia kipato lakini kwa pamoja ni rahisi kutimiza lengo hilo.

Ni vyema nchi wanachama EAC kushirikiana kwa kuwa na tamko la pamoja na wanasheria wa jumuiya kutetea uamuzi wa serikali ikiwa itatokea kupelekana katika vyombo vya dola.

Hiyo itasaidia kufikia malengo kwa haraka kwa nchi zote kuliko kusubiri kila mtu kushughulikia kipekee, kwani itachelewesha makubaliano hayo kutokana na sababu mbalimbali ikizingatia nchi hizo zinatofautiana masuala mengine.

Kama kuna jambo nchi hizo zimekubaliana na ikatokea nchi nyingine kusuasua ni vyema zikajadili kwa pamoja ili kufikia malengo.

Nasema hivyo kutokana na kuwa nchi hizi zimepakana na hufanya biashara huru hivyo nchi moja ikiwa na bidhaa ambayo jumuiya ilikubaliana kuiondoa katika mzunguko, ni vigumu nyingine kusimamia usitishwaji wake.

Pamoja na kuwepo kwa tofauti ya uchumi na nchi nyingine za EAC kuwa na changamoto za kisiasa, kukubaliana tu kuondoa suala fulani bila ushirikiano wa pamoja ni vigumu. Ni vizuri kila nchi ichukue suala hilo kwa uzito unaostahili.