Sumatra, Polisi Mwanza zimulikeni daladala hizi

KWA muda mrefu sasa kumekuwepo na kero ya baadhi ya madereva wa daladala za jijini Mwanza kukatisha safari na kusababisha usumbufu kwa abiria husika.

Tatizo hilo limekuwa likiendekezwa zaidi kati ya saa 2:00 na 4:00 usiku kwa baadhi ya daladala zinazofanya safari za Kisesa - Airport, Buhongwa - Kisesa, Buhongwa - Airport, Kishiri - Airport, Buhongwa - Kishiri, Bwiru - Machinjioni na Kisesa - Bwiru.

Baadhi ya madereva na makondakta wa daladala hizo wamekuwa wakiwatelekeza abiria na mizigo yao njiani nyakati za usiku bila kujali nauli wanazokuwa wamepokea kwa ajili ya kuwafikisha mwisho wa safari zao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya abiria wanaokatishiwa safari hizo wamekuwa wakilazimika kutumia fedha nyingine nje ya bajeti yao kugharimia usafiri mwingine wa kuwafikisha mwisho wa safazi zao.

Wakati mwingine baadhi ya abiria wanaotelekezwa njiani wamekuwa wakikumbwa na mikasa ya kuvamiwa na kukabwa na vibaka ambao huwapora mali mbalimbali zikiwamo fedha na simu za mkononi.

Malalamiko ya abiria kukatishiwa safari nyakati za usiku jijini Mwanza yamekuwa yakiripotiwa kwenye mamlaka husika, lakini bado hakuna hatua thabiti zilizochukuliwa kukomesha tatizo hilo.

Vyombo vyenye dhamana ya kusimamia huduma za usafirishaji ni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na kwa upande mwingine, askari polisi wa usalama barabarani.

Kuna haja ya mamlaka hizo kuongeza juhudi za kufuatilia na kutoa adhabu stahiki dhidi ya wamiliki, madereva na makondakta wa daladala zinazokatisha safari kwani vitendo hivyo vinawapora abiria haki zao.

Sambamba na hilo, Sumatra na trafiki washughulikie pia tatizo linaloonekana kuwa sugu la makondakta wa daladala kutotoa tiketi kwa abiria wanaolipa nauli jijini Mwanza. Ni dhahiri kuwa uwezo wa kukomesha kero hizo upo mikononi mwa viongozi na watendaji wa mamlaka hizo jijini Mwanza.

Wakiamua inawezekana. Itapendeza zaidi kuona abiria wa daladala za jijini Mwanza wanatendewa haki ya kupewa tiketi na kufikishwa mwisho wa safari zao bila kutelekezwa njiani huku wakiwa tayari wameshalipa nauli husika.

Chonde chonde viongozi na watendaji husika, ungeni mkono kwa vitendo kauli ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu kwa kuchukua hatua za makusudi kukomesha kero hizo jijini Mwanza. Penye nia pana njia.