Juhudi zinahitajika kuzuia mimba kwa wanafunzi

TATIZO la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, bado limekuwa ni changamoto kubwa katika baadhi ya mikoa nchini na hivyo kutishia maendeleo ya elimu nchini.

Hali hii imekuwa ikirudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha watoto wote, wanapatiwa elimu ya msingi na sekondari; na pia imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya mwanafunzi husika kwa kukatisha ndoto zake na malengo ya maisha yake ya baadaye.

Sote tunajua kwamba tatizo la mimba za utotoni, lipo katika jamii zote duniani na mbali na kuathiri afya za watoto hao, pia huathiri ndoto za maendeleo ya watoto wa kike, wanaokumbwa na tatizo hilo pamoja na familia zao.

Tunaambiwa kwamba idadi ya wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya mimba katika shule za msingi na sekondari nchini, imeongezeka kutoka takribani watoto 3,000 mwaka 2013 hadi wanafunzi 5,033 mwaka 2016.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita mimba za utotoni na rushwa mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Watoto katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai alisema ongezeko hilo, linatishia maendeleo ya elimu nchini.

Kutokana na hilo, ni wazi kwamba jambo hili, bado linahitaji juhudi za wote ili kuhakikisha tatizo hili la mimba kwa wanafunzi linakwisha na kuwawezesha watoto kupata haki zao zote za msingi, ikiwemo elimu bora bila kukutana na vikwazo.

Ni wazi kwamba katika maeneo yetu, tumeshuhudia wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na tatizo hili la mimba, wanazozipata wakiwa shuleni. Watoto hao wengi wao wamekuwa wakikosa mwelekeo baada ya kupata ujauzito na hiyo inatokana na sababu mbalimbali.

Hapa nchini wanafunzi wanapopata mimba inakuwa ndiyo mwisho wa elimu yao kwa upande wa shule za serikali, labda kama mzazi au walezi wana uwezo wa kumpeleka na kumuendeleza mtoto huyo na masomo yake katika shule binafsi.

Tunafahamu kwamba watuhumiwa au watu wanaohusishwa na matukio ya kuwapa mimba wanafunzi, wengine wamekuwa wakilindwa na jamii, jambo ambalo si sahihi na limekuwa likirudisha nyuma juhudi za kukabiliana na watu hawa.

Hivyo kutokana na changamoto hii, ni vyema wote tukashirikiana na kuhakikisha kwamba tunakomesha mimba hizi kwa wanafunzi; na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Pia elimu zaidi ikiwemo ya afya ya uzazi, inapaswa kutolewa kwa watoto wetu, hasa wawapo shuleni ili kuhakikisha kwamba wanafahamu pia madhara yatokanayo na mimba za utotoni.

Jamii pia inapaswa kutoa ushirikiano, pale anapotokea mtu anatuhumiwa kuhusika na masuala kama hayo ya kuwapa mimba wanafunzi na kuhakikisha kwamba anafikishwa katika vyombo vya sheria.

Naamini kwamba kama kila mtu atasimama katika nafasi yake, mimba kwa wanafunzi zitakoma.