KAMPUNI na wafanyabiashara kutoka India wataendelea kuwa waagizaji wakubwa na wanunuzi wa nafaka na mazao mchanganyiko, yakiwemo ya viungo kutoka Tanzania.
Balozi wa India hapa nchini, Binaya Srikanta Pradhan amesema hayo wakati wa majadiliano ya kukubaliana na kuweka ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi za nchini, India ikiwemo taasisi ya Teknolojia India (ITI).
Amesema Tanzania ni sehemu muhimu ambayo inazalisha mazao ya aina mbalimbali yakiwemo ya korosho, soya , maharagwe mabichi, parachichi na yale ya viungo ambayo mengi hununuliwa na kampuni kutoka India .
Pradhan amesema ushirikiano na SUA utaiwezesha India kufungua milango ya kubadilishana wataalamu kati ya taasisi za vyuo vikuu vya nchini mwake kwenye sekta ya uhandisi kilimo, mifugo na uvuvi na uhandisi katika kilimo cha umwagiliaji.
Amesema kuwa hatua hiyo itawezesha kuboreshwa uzalishaji katika nyanja hizo na hivyo kusaidia kuimarisha masoko ya nchini India , kukabiliana na changamoto za ubora wa bidhaa zinazozalishwa, ili kupata soko la uhakika nchini humo.
“ Ujio wangu SUA unanipa fursa ya kuangalia vitu gani tunaweza kuvifanya kwa pamoja ili kuunganisha sekta ya kilimo, tafiti, masoko, mafunzo na teknolojia katika nchi hizi mbili kwa manufaa ya wananchi wa pande zote “ alisema Balozi Pradhan.
Balozi Pradhan amesema faida aliyoipata mara baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya Chuo Kikuu hicho hususani eneo la Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Wanyama na Kituo cha Utafiti wa Uchumi wa Buluu, imeonesha ya kwamba SUA imejizatiti katika kuleta maendeleo ya kilimo nchini Tanzania.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Raphael Chibunda ametaja kuwa mkakati wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo ya chuo hicho kitakuwa cha kuzalisha watu wanaoenda kutengeneza kazi .
Profesa Chibunda amesema kwa sasa tayari Chuo Kikuu kimekuwa na Atamizi, kufanya maboresho ya mitaala pamoja na kuweka mkazo kwa wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo.