India yaanza kuondoa wanajeshi wake Maldives

NEW DELHI, Maldives: TAARIFA ya Rais wa Jamhuri ya Maldives Dk Mohamed Muizzu kwa wananchi wa taifa hilo kwamba wanajeshi wa India hawatakuwepo katika taifa hilo baada ya Mei 10 zimeanza kutekelezwa baada ya India kuanza kuwaondoa wanajeshi wake wanaoendesha ndege za uchunguzi huko Maldives.

Ripoti za vyombo vya habari nchini humo vinaeleza kwamba wanajeshi 25 wa India waliotumwa katika kisiwa cha Kusini Addu nchini humo wameondoka katika visiwa hivyo kama sehemu ya makubaliano ya nchi hizo mbili.

Awali Dk Muizzu alitangaza jambo hilo katika hotuba yake ya kwanza kwa Bunge mnamo Februari 5 na kuirudia siku chache kwamba wanajeshi wa India watarejeshwa kutoka taifa hilo baada ya Mei 10.

Advertisement

Taarifa ya awali zilieleza kwamba timu ya raia wa India ilichukua jukumu la kuendesha ndege katika anga la taifa hilo, kabla ya tarehe ya mwisho iliyokubaliwa na mataifa hayo mawili kuwaondoa wanajeshi wa India.

“Hakutakuwa na wanajeshi wa India nchini ifikapo Mei 10, wakiwa katika mavazi ya kiraia ama mavazi ya kijeshi.

Jeshi la India halitakuwa likiishi katika nchi hii kwa aina yoyote ile, nasema hili kwa kujiamini kabisa,” amesema Rais Muizzu baada ya hivi karibuni kutia saini ya makubaliano na China ya kupokea msaada wa kijeshi wa bure.

Amesema kwamba kupata uhuru wa kweli ni dhana anayoichukulia kwa kipaumbele kikubwa ndiyo maana anaendelea na juhudi ili kufanikisha jambo hilo la kuwaondoa wanajeshi wa India nchini mwake pamoja na kurejesha eneo la bahari ambalo nchi yake ilinyimwa.

“Naamini tunaweza kufanya hivyo. Kuchelewa kuhitimisha kazi hii kulitokana na taratibu mbaya zilizofanyika wakati wa utekelezaji ambapo ilifanyika bila kupeleka suala hilo bungeni jambo ambalo ni kinyume na Katiba,” ameeleza rais Muizzu.