KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa mwaka 2021-2022 kilisajili jumla ya miradi 630 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.74 kutoka kwa wawekezaji kutoka India na katika uwekezaji huo ajira zilizopatikana mpya ni zaidi ya 60,000.
Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax katika Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na India katika uchumi, teknolojia na sayansi.
Katika mkutano huo ambapo mataifa yote mawili yalitia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali takwimu zikionesha biashara baina ya mataifa hayo mawili inapaa na kufikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.476 mwaka 2023. Maeneo ambayo wameingia makubaliano zaidi kwa sasa ni kwenye siasa, biashara, uwekezaji, maji, elimu, nishati, afya, tehama na masuala ya ulinzi.
“Tunafanya vizuri kwenye biashara na uwekezaji, India ni mbia wetu mzuri wa biashara anachukua nafasi ya nne kibiashara hapa nchini na katika uwekezaji anashika nafasi ya tano, tuna ushirikiano mzuri wa manufaa kwa pande zote,” alisema Dk Tax.
Akizungumzia ushirikiano katika maeneo hayo, Dk Tax alisema mfano katika sekta ya maji, India itashirikiana na Tanzania kupata msaada wa kuboresha upatikanaji wa maji katika Mji wa Dodoma.
Awali akizungumza mara baada ya kutiliana saini mikataba hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Dk Subrahmanyam Jaishankar alisema mataifa hayo mawili yanafurahia ushirikiano wao wa muda mrefu na unaozidi kuimarika.
“Tunaendelea kuimarisha uhusiano wetu, tumezungumzia maeneo mapya ya ushirikiano kama sekta ya maji, teknolojia na masuala ya kuimarisha ujuzi, tutaendelea kushirikiana pia katika ngazi za kimataifa,” alisema Dk Jaishankar na kuongeza kuwa Tanzania ni moja ya mataifa yanayokuwa kiuchumi barani Afrika.
Takwimu za biashara kutoka ubalozi wa India, zinaonesha mwaka 2022-2023 mataifa hayo yalifanya biashara ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.476 huku mwaka uliotangulia wa 2021-2022 biashara ilifika Dola za Marekani bilioni 3.139 na mwaka 2017-2018 ilikuwa Dola za Marekani bilioni 2.647.