Intaneti kuboreshwa UDSM

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), kimesaini mkataba wa kihistoria wa marejeo na Kampuni ya Seacom kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma ya inteneti chuoni hapo.

Katika marejeo hayo ya kimkataba, UDSM imefanikiwa kuongeza uwezo wa intaneti itakayopatiwa na kampuni ya Seacom kutoka Megabaits 155 kwa sekunde hadi kufikia Gigabaits 10 kwa sekunde.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema mkataba huo ni muhimu kwa maslahi mapana ya Chuo.

Advertisement

“Dira ya Chuo ya mwaka 2061 inakielekeza Chuo kutumia teknolojia katika kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji.

“Kwa kutumia mwelekeo huo, Chuo kina mpango wa kuwa na kampasi maizi ‘Smart Campus’, Uwepo wa intaneti yenye kasi kubwa unakiwezesha Chuo kutimiza ndoto yetu ya kuwa kampasi maizi,” amesema.

Kwa upande wake amesema baada ya kuboresha miundombinu husika, huduma hiyo ya Intaneti yenye kasi kubwa itapatikana katika Kampasi zote hata zile zilizo nje ya Dar es Salaam, ikiwemo ya Zanzibar, Dodoa, Nzega, Mbeya na Kampasi mbili mpya za Lindi na Kagera.

Amesema kwa kutumia uwezo huo wa Intaneti yenye kasi kubwa, UDSM itaweza kutekeleza dhamira yake ya kuwa KAMPASI MAIZI “SMART CAMPUS” ambapo shughuli muhimu za Chuo zinatarajiwa kufanyika kwa njia ya mtandao.

“Kwa kutumia kasi kubwa ya intaneti itakayopatikana, tunatarajia ufanisi wa Chuo katika Ufundishaji, Utafiti na huduma kwa umma utaongezeka.

“Kwa maana nyingine, uwezo wetu wa kuwahudumia wanafunzi, watafiti na jamii kwa ujumla utaongezeka na huduma zetu zitakuwa bora zaidi,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Seacom (TZ), LTD Joe Vipond amekiri kampuni hiyo kuchukua muda kufikia makubaliano hiyo kwa lengo la kuboresha huduma hiyo chuoni.

Amesema kwa kufikia hatua hiyo ni faida kubwa kwa chuo na wanafunzi.

Mwisho