MIKAKATI ya Serikali ya kuvutia wawekezaji imewezesha Kampuni ya ITRACOM FERTILIZERS ya Burundi kuwekeza kiwanda cha saruji mkoani Kigoma.
Hayo yamebainishwa bungeni leo na Naibu Waziri, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe wakati wa kujibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, Nashon Bidyanguze(CCM).
Katika swali lake, Bidyenguze alitaka kujua ni lini Serikali italeta mwekezaji wa kiwanda cha sementi katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Akijibu swali hilo, Kigahe amesema Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhamasisha na kuvutia wawekezaji ikiwemo kwenye sekta ndogo ya saruji nchini.
Amesema Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Kigoma kimeweza kuvutia Mwekezaji (ITRACOM FERTILIZERS CO. LTD) kujenga kiwanda cha saruji.
Kigahe amesema kuwa pia mwekezaji huyo amepewa ekari 47 za ardhi katika Eneo la Uwekezaji la Kigoma (KiSEZ) na kuwa
Wilaya ya Uvinza pia itanufaika na mwekezaji huyo.
Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji zaidi ili kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma ikiwemo Wilaya ya Uvinza.