KATIKA siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio yasiyo ya kawaida na yasiyo ya kibinadamu yanatokea katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiacha familia na jamii katika maumivu na sintofahamu ya kutaka kujua nini hasa kinaendelea au nini sababu ya matukio hayo.
Matukio ya mauaji, ubakaji na unyanyasaji miongoni mwa jamii yameongezeka kwa kiwango kikubwa yakihusisha uhusiano wa mapenzi, ushirikina, visasi, ugomvi wa familia kwa ajili ya mali na wengine wakijitoa uhai kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.
Imekuwa kawaida sasa kusikia mwanaume kamuua mkewe, mwanamke kamuua mumewe, huyu kamchoma moto yule, baba kambaka mtoto wa kumzaa, kaka kambaka dada yake. Wakati mwingine ni imani za ushirikana zinasababisha mauaji baina ya ndugu na majirani wakituhumiana uchawi.
Maswali mengi yanaibuka vichwani mwa watu lakini binafsi najiuliza ulimwengu unakwenda wapi?
Watu wamezipa mgongo imani za dini zao? Wamemsahau Mungu na hawana hofu tena ya kutenda dhambi? Majibu yanakuwa magumu kupatikana katika mtazamo wa juu juu.
Katika matukio yote hayo jamii imekuwa ikirusha lawama kwa wale wanaotenda hivyo vitendo vya ukatili na visivyo vya kawaida kwa kuwaona wabaya bila kujaribu kuchunguza kwa ndani ni kwanini wanafikia kufanya hivyo. Je, ujasiri wa namna hivyo unajengwa na nini ndani yao? Je, akili zao ziko katika hali ya kawaida na kiwango cha kawaida cha kufanya kazi na kusaidia kufanya uamuzi kwa usahihi katika matendo ya maisha yao?
Kiuhalisia mwananadamu anapaswa kuwa na nafsi iliyo hai katika kila uamuzi anaoufanya katika maisha yake, kuanzia uamuzi binafsi hata uamuzi unaohusiana na watu wengine wa karibu yake na wasio wa karibu yake kwa kuwa nafsi hai humwongoza mtu kutenda matendo mema na kumuonya pale ambapo anaenda kutenda ubaya.
Kila kitu mtu anachopaswa kukifanyia uamuzi ni lazima ajiulize maswali kadhaa ya muhimu, je, nini itakuwa matokeo yake, yana faida au hasara, nini madhara yake kwangu na kwa wengine ukiona huwezi kujiuliza hayo maswali au unajiuliza lakini baadaye unaamua kuyapuuza ujue kuna walakini kwenye uhai wa nafsi yako na afya ya akili yako.
Ili nafsi iwe hai inahitaji utulivu wa akili na afya ya akili hivyo mtu yeyote anayesumbuliwa na mawazo ya kupita kiasi bila kupata msaada wa aina yoyote husababisha msongo wa mawazo, kutetereka kwa uhai wa nafsi na kumfanya mtu kuwa katili na mbinafsi asiyejali maumivu ya wengine wala kutofautisha matendo mema na mabaya.
Uovu na vitendo vya ukatili ambavyo jamii inavishuhudia nyakati hizi ni matokeo ya tatizo kubwa la afya ya akili ambalo jamii hii inakabiliana nalo kwa sasa lakini imeamua kufumba macho kana kwamba hakuna kinachotokea kuanzia katika ngazi ya familia.
Kuna wakati familia inaona mmoja wa wanafamilia amebadilika kitabia, amekuwa mpole kupitiliza, mtu wa kujitenga, mkimya sana au wakati mwingine anakuwa mtu wa kuongozwa na hasira na kulipuka kila wakati lakini wanaishia kumshangaa na kumlaumu kwa mabadiliko hayo bila kutaka kujua sababu.
Mtu ataendelea kupambana na maumivu ya moyo na nafsi huku akiendelea kuathiri afya ya akili yake bila msaada kwa sababu anaona hata akiwaeleza ndugu au marafiki wa karibu watamwongezea shida badala ya kumsaidia kwa sababu ni kawaida kwenye jamii yetu kuona mtu anaelezwa tatizo la mtu ambalo angehitajika kulitatua kimya lakini yeye analiacha bila utatuzi na anachukua jukumu la kulisambaza na kumwongezea mhusika uchungu.
Mtu anayeanza kupata tatizo la afya ya akili hasa kutokana na msongo wa mawazo au uchungu wa aina yoyote, anapaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa kwa upole na kufarijiwa badala ya kupewa lawama au kuhukumiwa. Jamii kwa sasa inatakiwa kuvalia njuga tatizo hili kwa kila mmoja kutafuta elimu ya afya ya akili na namna ya kukabiliana nayo na wale wenye taaluma hiyo wawe tayari kusaidia wengine.
.