Ireland yatoa Sh bil.4.6 uchumi wa buluu

SERIKALI ya Ireland imetoa fedha kiasi cha Sh bil 4.6 kwa ajili ya kusaidia serikali ya Tanzania katika juhudi za uchumi wa buluu.

Fedha hizo zitatekelezwa kupitia mradi wa Bahari Mali katika mikoa ya Tanga na Pemba, ambapo itasaidia kuwezesha kiuchumi vikundi 19 vya vijana na wanawake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, David Silinde amesema kuwa mradi huo unakwenda kuwajengea uwezo wananchi wanaoishi maeneo ya ukanda wa Pwani.

Amesema kuwa kupitia mradi huo wananchi wataweza kunufaika na fursa ya elimu ya ujasiriamali, lakini na namna ya kutumia fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu katika kujiimarisha kiuchumi.

“Ukosefu wa mitaji, maarifa ya biashara ni miongoni mwa changamoto ambazo zinasababisha wananchi wetu kushindwa kunufaika na fursa zilizopo katika uchumi wa bahari, sasa kwa mradi huu tunaenda kumaliza changamoto hiyo,”amesema Naibu Waziri huyo.

Amesema kuwa vikundi vya wananchi wanaojishughulisha na kufanya shughuli katika maeneo ya bahari wanakwenda kunufaika kwa kupatiwa mitaji kupitia mikopo isiyo na riba, ili waweze kujiendeleza kiuchumi.

Naye Kaimu Balozi wa Ireland nchini, Mags Gaynor amesema kuwa mradi huo una lengo la kusaidia wananchi wa Tanzania kuhakikisha wanafikia ndoto yao ya uchumi wa buluu.

“Kupitia mradi huu sasa wananchi wataweza kunufaika na fursa zilizopo katika bahari, lakini na kulinda mazingira ya bahari, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,”amesema Gaynor

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x