FAMILIA ya Chifu Mkwawa kwa kushirikiana na baadhi ya wadau leo katika ngome yao iliyopo Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa inaanza kufanya sherehe kumbukumbu ya kiongozi huyo wa kabila la wahehe ikiwa ni miaka 125 tangu kufariki kwake.
Historia inaonesha Mkwawa alizaliwa mwaka 1855 katika kijiji cha Luhota Iringa Vijijini na alifariki kwa kujiua mwenyewe mwaka 1898 akiwa na miaka 42 tu baada ya kuhofu kuuawa na watawala wa kijerumani aliopigana nao kulinda utawala wake.
Kumbukumbu hiyo ambayo mgeni rasmi wake atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego inatarajiwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, viongozi wa serikali na machifu kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Gwanda amechangia kilo 200 za mchele katika kuunga mkono familia hiyo na wadau wake kufanikisha shughuli hiyo iliyochangiwa na wadau wengine pia akiwemo Salim Asas.
Akipokea msaada wa chakula hicho, Fatma Mkwawa ambaye ni kitukuu wa chifu huyo alisema; “Kwa mara ya mwisho shughuli za kumkumbuka ya chifu huyo zilifanyika mwaka 1999.”
Alisema katika hafla hiyo iliyoongozwa na babu yake Chifu Adam Sapi Mkwawa aliyekuwa Spika wa kwanza wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mgeni rasmi.
“Kuanzia sasa shughuli hii itakuwa endelevu na itakuwa ikifanyika kila mwaka kati ya Juni 17 na 19 kwa lengo la kumuenzi na kumkumbuka shujaa wetu,” alisema.
Alisema shughuli hiyo ya kumbukumbu itakuwa ikiongozwa na chifu wa sasa wa wahehe, Chifu Adam Abdul Sapi Mkwawa wa Pili ambaye ni mdogo wake wa tumbo moja pamoja na wazee wa kimila wa kabila la kihehe.