WAKATI baadhi ya wadau wakionekana kutozihafiki takwimu zinazoonesha mkoa wa Iringa unaongoza kwa udumavu nchini, mkoa huo umetangaza kuyatumia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mwaka huu kuzindua mkakati wake wa miaka mitano wa kukabiliana na changamoto hiyo.
Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2023, Mkuu wa Mkoa alisema; “Takwimu za udumavu nchini zinaonesha mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na asilimia 56.9 ya watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu.”
Mkoa wa Iringa unafuatiwa na mkoa wa Njombe wenye asilimia 50.4 na Rukwa wenye asilimia 49.8 pamoja na kwamba ripoti ya utafiti wa Hali ya Uzazi ya Afya ya Mama na Mtoto na Maralia inaonesha kuwa hali ya udumavu nchini imepungua hadi asilimia 30 mwaka 2022.
“Hii maana yake kwa kila watoto 10 mkoani mwetu, wastani wa watoto sita wana udumavu. Tunakuja na mkakati wa miaka mitano wa kukabiliana na changamoto hii. Tunaomba wadau wote mtuunge mkono katika kutekeleza mkakati huo,” alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema mkakati wa kukabiliana na udumavu utahusisha utoaji wa elimu ya lishe bora, matumizi ya vyakula vyenye lishe bora kwa wanawake wajawazito na watoto, upatikanaji wa maji safi na salama, na ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto.
Mengine ni pamoja na uwekezaji katika kilimo bora ili kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye lishe bora, kuendesha kampeni zinazohusiana na afya na udumavu ili kuongeza uelewa, kuboresha hali ya maisha ya wanawake na kushughulikia sababu za kijamii na kiuchumi.
“Tusikubali kubaki nyuma wakati uwezo wa kusadia watoto wetu tunao. mkakati tunaokwenda kuuzindua Machi 8 mwaka huu utahusisha wazazi, walezi, walimu, wataalamu wa afya, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla,” alisema.
Hata hivyo baadhi ya wadau akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Steven Mhapa wamehoji sababu za mkoa wa Iringa kuongoza kwa takwimu hiyo huku ripoti nyingine za mendeleo ya mtoto zikionesha hali tofauti.
Kama watoto wanaougua udumavu wanaweza kukabiliwa na ucheleweshaji wa maendeleo ya akili na kimwili na kuathiri uwezo wao wa kujifunza shuleni, Mahapa aliuliza, inawezekanaje watoto hao wakawa na ufaulu mzuri katika mitihani yao mbalimbali.
“Mnawezaje kuwa na mkoa wenye takwimu za juu za udumavu halafu ukija kwenye maendeleo yao shuleni na ufaulu wao viwango ni vya juu sana?” Mhapa aliuliza huku akifanya rejea ya jinsi mkoa wa Iringa unavyofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya shule za msingi na sekondari.
Akizungumzia utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi hicho, Mkuu wa Mkoa alizipongeza halmashauri zote za mkoa huo kwa kutekeleza afua mbalimbali za lishe kwa kuzingatia viashiria vilivyomo katika mkataba huo na kuhakikisha huduma bora za lishe zinaztolewa ili kuondokana na matatizo ya utapiamlo hususani udumavu.
Akizungumzia mafanikio ya jumla katika utekelezaji wa mkataba huo, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Iringa Anna Nombo alisema kumekuwa na mwitikio wa mkubwa wa viongozi wa ngazi zote katika kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mkataba jambo linalotoa mwelekeo chanya wa utekelezaji wa viashiria vyake.
Kwa kupitia kiashiria cha matone ya Vitamini A alisema zaidi ya watoto 57,000 walifikiwa katika kipindi hicho na kati yao, watoto 248 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali, 245 walipatiwa matibabu na kupona huku watatu wakifariki dunia.
Kuhusu kishiria cha elimu ya ulishaji watoto wachanga na watoto wadogo kupitia watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya, Nombo alisema imevuka lengo kwani imetolewa kwa asilimia zaidi 154 kwa wazazi na walezi waliohudhuria kliniki za uzazi na mtoto (RCH).
Katika kiashiria cha utoaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari alisema, kati ya shule 756 ni shule tano tu zikiwemo nne kutoka wilaya ya Mufindi na moja Kilolo ambazo hazitoi chakula.
Mkuu wa Mkoa alizikumbusha halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha chakula kinachotolewa kwa wanafunzi kuwa ni kile chenye viritubishi kwa utaratibu utakaowanufaisha wale wanaotoka katika kaya masikini.