Iringa yaanza kupata mafanikio kutokomeza udumavu

MKOA wa Iringa wenye asilimia 47 ya udumavu umetangaza kuanza kupata mafanikio katika utekelezaji wa afua za lishe zinazolenga kukabiliana na changamoto hiyo na utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Hali ya utekelezaji ni nzuri na inatia moyo, mkoa umetoka nafasi ya 10 mwaka 2020/2021 hadi kufika nafasi ya tatu 2021/2022 katika kupima na kutekeleza masuala mazima ya afua za lishe,” Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dengedo amesema.

Katika kupunguza udumavu kwa watoto mkoani humo Dendego alisema wameendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa lishe kutekeleza afua zinazoleta matokeo makubwa katika siku 1000 za kwanza za maisha ya mtoto.

Amezitaja afua hizo kuwa ni pamoja na kutoa matone ya madini ya chuma na asidi ya ‘folic’ kwa wakina mama wajawazito, kutoa matone ya Vitamini A na dawa za kutibu minyoo ya tumbo mara mbili kwa watoto wote wenye miaka chini ya mitano.

Alisema mkoa unaendelea kutoa matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wa umri huo,  kutoa elimu ya ulaji wa vyakula mchanganyiko na mtindo bora wa maisha unaolenga kuondokana na tabia bwete

Akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2022, Dendego alisema katika kipindi hicho watoto 557 wenye utapiamlo waliibuliwa na kuanza kupatiwa matibabu.

“Hata hivyo watoto 187 kati yao bado hawajapatiwa matibabu, nataka majibu kutoka kwa halmashauri zote zenye watoto hao nini kinawachelewesha na namna watakavyowapa huduma hiyo,” alisema.

Pamoja na watoto hao kutopata huduma, Dendego alisema bado halmashauri za mkoa wake zinasuasua katika kipengele cha utoaji fedha kwa asilimia 100 ili kutekeleza afua hizo za za lishe.

“Katika kipengele cha utoaji wa fedha bado tunalegalega; tumetoa asilimia 63 tu ya fedha nataka kuwaambia hili halikubaliki na natoa siku saba kwa wakurugenzi wa halmashauri zote watoe fedha hizo,” alisema na kuongeza kwamba jambo la utoaji wa fedha hizo sio la kusubiri au kuahirisha.

Alisema mikataba ya lishe waliosaini katika ngazi mbalimbali ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji wa afua mbalimbali za lishe katika jamii ili kupunguza kiwango cha udumavu.

Habari Zifananazo

Back to top button