MKOA wa Iringa umehimizwa kuongeza matumizi ya vyakula vilivyoongezwa virutubishi kibaiolojia na viwandani kama chumvi, mafuta ya kula, unga wa ngano na mahindi, na maharage lishe kama moja ya mikakati ya kupambana na tatizo la utapiamlo na udumavu.
Ukubwa wa tatizo la udumavu mkoani Iringa umeelezwa kuongezeka huku taarifa mpya zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zikionesha kati ya watoto 100 wenye miaka chini ya mitano, 56 wana changamoto hiyo.
Akitoa taarifa hiyo leo kwenye mkutano wa kufunga awamu ya kwanza ya mradi wa vyakula vilivyoongezewa lishe kibaologia, Mkurugenzi Msaidizi wa Tamisemi anayeshughulika na huduma za lishe, Mwita Waibe alisema;
“Hali ya udumavu katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususani mkoa wa Iringa inazidi kuongezeka na kuacha maswali mengi kwa kuzingatia kwamba mkoa huu ni moja ya mikoa inayozalisha kwa wingi vyakula vya aina mbalimbali na matunda.
Katika kukabiliana na hali hiyo Waibe alisema serikali imaemua kufanya tathmini ya haraka ili kujua mkoa huo na mingine ambayo hali hiyo haipungui ina changamoto gani za ziada ili zishughulikiwe kwa kasi zaidi.
Aidha alisema mipango ya serikali katika mapambano hayo inalenga kuziwezesha halmashauri zote nchini zinakuwa na maafisa lishe kati ya watatu na wanne watakaohakikisha huduma, taarifa na shughuli mbalimbali zinazohusu lishe zinatekelezwa kwa wakati.
Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Mhandisi Leonard Masanja alisema serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuboresha afya na lishe kwa kupitia shule na jamii na katika tathmini ya mkataba wa lishe iliyofanyika Dodoma, Rais Dk Samia Suluhu Hassan alisisitiza matumizi ya vyakula vilivyoongezewa virutubishi.
Meneja Mradi wa Urutubishaji Vyakula wa Shirika la GAIN Tanzania, Edwin Josia alisema kwa miaka minne katika mikoa tisa ya Iringa, Ruvuma, Songwe, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Geita, Kigoma na Kagera wamekuwa wakitekeleza mradi huo unaolenga kuboresha uzalishaji na utumiaji wa mazao yaliyoongezewa viinilishe kibaiolojia.
Aliyataja mazao makuu yanayozaliswa kupitia mradi huo ambao awamu yake ya kwanza imekwisha kuwa ni mahindi lishe ambayo yana wingi wa vitamin A na maharage lishe yenye wingi wa madini chuma na zinki ambayo kwa pamoja yanasaidia kukabiliana na utapiamlo na udumavu.
“Mradi umefanikiwa kutoa elimu kwa wajasiliamali 86 katika mikoa hiyo tisa juu ya upatikanaji wa mahindi na maharage lishe, umuhimu wa mazao hayo na bidhaa mbalimbali zinazoweza kupatikana kutoka katika mazao lishe,” alisema.
Kwa upande wa shule, Josia alisema mradi umefanikiwa kutoa elimu kwa wakuu wa shule 151 katika mikoa hiyo na kati yake shule 96 zinatumia maharage lishe, mahindi lishe au vyote.
Alisema mkoa wa Iringa ni wa kujivunia zaidi kwani mradi huo umeweza kuzifikia shule 71 na kati yake 54 zinatumia mazao lishe hayo.
Naye Mkuu wa Programu za GAIN, Dk Winfrida Mayilla alisema matarajio ya shirika lao ni kuona wafanyabiashara wanaendelea kusambaza vyakula vya lishe masokoni na mashuleni ili kusonga mbele katika kupiga vita utapiamlo.
Mmoja wa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula lishe kwa kupitia GAIN, Beatrice Msafiri alisema kwa kupitia mradi huo waliwezeshwa kupata mashine za kuzalishia unga na kuunganishwa na wakulima wanaozalisha maharage na mahindi.
Alisema nafaka lishe hazina changamoto zozote za kiafya kama baadhi ya watu wanavyoamini bali zinavirutubishi vyote muhimu katika kukabiliana na utapiamlo na udumavu.