“Ukifika Mjini Iringa na kujionea jinsi Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) inavyoboresha huduma hizo kwa watu wote utabaini namna inavyofanikiwa kutekeleza ajenda ya 2030 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),” anasema Wigeli Mgimwa.
Ajenda ya 2030 na lengo namba sita la SDGs vinaleta masuala ya ubora wa maji mstari wa mbele katika hatua za kimataifa zinazolenga kuhakikisha upatikanaji na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ili kuzikabili changamoto zinazohusishwa na masuala ya maji.
Huduma za maji zinafanunuliwa chini ya SDGs nyingine kama vile afya, kupunguza umaskini, mifumo ya ikolojia na matumizi endelevu na uzalishaji, uhusiano kati ya maji na masuala muhimu ya mazingira, jamii, uchumi na maendeleo.
Mgimwa ambaye ni fundi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) cha mjini Iringa anayeshghulikia huduma ya maji anasema; “Tunapata maji kila siku na kwa saa 24. Hii imewafanya baadhi ya wanafunzi wasiwe na matumizi sahihi ya maji wakidhani huduma ya maji chuoni hapa ni ya bure na hivyo kukipa chuo mzigo mkubwa wa bili.”
Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA, Mhandisi David Pallangyo anasema IRUWASA ilianzishwa kwa Sheria ya Maji Na 8 ya mwaka 1997 Julai mosi mwaka 1998 ikiwa daraja C; mwaka 2003 ikapanda daraja B na mwaka 2007 hesabu zake zilipoonesha ina uwezo wa kumudu gharama zake za uendeshaji, matengenezo na kuchangia uwekezaji ikapandishwa na kuwa daraja A.
Mkurugenzi wa Iruwasa, David Pallangyo
“Mwaka 2020 IRUWASA iliongozewa eneo la kutoka huduma katika mji wa Ilula na Kilolo wilayani Kilolo, lakini pia kutokana na mtandao wetu kuwa mkubwa tumepewa maeneo ya pembezoni mwa Iringa katika halmashauri ya wilaya ya Iringa ili nayo tuweze kuyahudumia,” anasema Mhandisi Pallangyo.
Wakati Dira ya IRUWASA ni kuwa Mamlaka kinara katika kutoa huduma endelevu ya majisafi na salama pamoja na usafi wa mazingira kwa viwango vya kimataifa, Mhandisi Pallangyo anasema dhima ya mamlaka hiyo ni kutoa huduma bora ya majisafi na salama na usafi wa mazingira ili kuinua hali ya maisha ya wakazi wa Manispaa ya Iringa.
Anasema asilimia 97 ya wakazi zaidi ya 200,000 wa manispaa hiyo na maeneo ya pembezoni mwa mji huo wanapata huduma ya majisafi kwa wastani wa saa 23 na hivyo kuvuka lengo la kitaifa na malekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 yanayotaka ifikapo mwaka 2025 huduma ya majisafi iwafikie asilimia 95 wakazi wote wa mjini.
Anasema asilimia tatu ya wakazi wa manispaa ya Iringa ambao hawajafikiwa na huduma ile ni wale walioko katika maeneo yenye asili ya vijiji na kwamba ifikapo 2025 huduma katika mji huo itakuwa kwa asilimia 100.
“Tuna wateja zaidi ya 42,000 Iringa Mjini wanaopata huduma kupitia matangi 18 ya kuhifadhi maji yanayochukua mita za ujazo 8,735 na mtandao wa mabomba wenye vipenyo mbalimbali (63mm-500mm) wenye urefu wa zaidi ya kilometa 724,” anasema.
Kwa upande wa mji wa Kilolo na Ilula ambako huduma yao imefika kwa asilimia 80, Mhandisi Pallangyo anasema Kilolo wana wateja zaidi ya 1,160 na vituo vya maji 50 na Ilula kuna wateja zaidi ya 1,850 na vituo 57.
Kuhusu kiasi cha maji yasiyolipiwa (yanayopotea) kwasababu mbalimbali zinazoendelea kufanyiwa kazi ikiwemo ya uchakavu wa mabomba, wizi wa maji, utendaji hafifu wa mita za wateja na uharibifu wa mtandao wa maji anasema kimepungua hadi wastani wa asilimia 22 tofauti na wastani wa kitaifa wa asilimia 37.
“Na kwa upande wa huduma ya maji taka tumefikia asilimia 10 tukiwa na wastani wa wateja 2,400. Tuna mfumo wa uondoaji majitaka wenye mtandao wa mabomba yenye urefu wa kilometa 72, mabwawa saba ya kutibu majitaka, mabwawa jengwa ya ardhi oevu mawili na magari mawili ya uondoaji majitaka,” anasema huduma hiyo inatakiwa kufika asilimia 30.
Anasema ili wafikie lengo la asilimia 30 wataongeza mtandao wa kuondoshea maji taka na kujenga mabwawa mawili ya kutibu majitaka katika kijiji cha Kiwele na Kipululu kupitia mradi mkubwa wa majisafi na majitaka utakaojengwa kwa Dola milioni 88.4 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 200.
“Katika kuthamini utendaji wa mamlaka za maji na kusema ipi inafanya vizuri zaidi Ewura wanaangalia kiwango na muda wa upatikanaji wa maji katika eneo husika, kiwango cha maji yanapotea na huduma ya uondoshaji majita taka,” anasema.
Anasema kwa kupitia vigezo hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeitangaza IRUWASA kuwa mamlaka ya kwanza kati ya mamlaka 26 za miji mikuu ya mikoa nchini kwa utoaji wa huduma za maji safi na uondoshaji wa maji taka kwa mwaka 2021/2022.
Anasema tuzo hiyo na zingine walizopata miaka ya nyuma imekuwa chachu ya kuwafanya wafanye kazi usiku na mchana kutimiza malengo yao huku azma ikiwa ni kuona wateja wao wanapata huduma kwa asilimia 100 na kwa saa 24 ifikapo mwaka 2025.
Kabla ya kupata ushindi huo Mhandisi Pallangyo anasema 2019/2020 walikuwa washindi wa tatu na mwaka 2020/2021 walikuwa washindi wa pili huku mwaka 2021/2022 wakiwa wa kwanza pia kati ya mamlaka hizo kwa ufungaji mzuri wa hesabu zinazokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na wakapata tuzo inayotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
“Kama kauli mbiu yetu inavyosema ‘Furaha Yako, Furaha Yetu’ IRUWASA inaamini huduma bora humfanya mteja kuwa na furaha, hulipia bili zake bila tatizo na hivyo kuisaidia IRUWASA kuendelea kuboresha huduma,” anasema na kuongeza kwamba kazi yao ni kuhakikisha wanaendelea kuwa wa kwanza nchini katika kutoa huduma hizo.
Mhandisi wa Uzalishaji, Martin Lusindiko anasema IRUWASA inatumia vyanzo vikuu vitatu kuzalisha maji kwa wateja wake ambavyo ni pamoja na Mto Ruaha Mdogo unaozalisha mita za ujazo 21,000 kwa siku, chemichemi ya Kitwiru mita za ujazo 3,000 na chemichemi ya Mawelewele mita za ujazo 330.
“Hivyo Mamlaka ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya mita za ujazo 24,000 ambazo ni zaidi ya lita 24,000,000 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa wakazi wote wa manispaa ya Iringa kwa siku ni wastani wa mita za ujazo 16,000 ambazo ni sawa na lita milioni 16 kwa siku,” anasema.
Mhandisi Lusindiko anasema mji wa Kilolo hutegemea vyanzo vya Ikunduvi, Mwosongela na Kiswengele vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa mita za ujazo 2,075 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya mji huo ya mita za ujazo 2,460 huku Ilula ikitegemea vyanzo vya Mgombezi, Ilomba na Idemle vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa mita za ujazo 6,300 ikilinganishwa na mahitaji ya mji huo ya mita za ujazo 2,900.
Mhandisi wa Uzalishaji, Martin Lusindiko
Anasema mamlaka ina kituo cha kusafisha na kutibu maji kilichopo eneo la Ndiuka, mjini Iringa yanayozalishwa na kusambazwa na IRUWASA yakiwa yanakidhi viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa.
Greyson Castory mkazi wa Kitasengwa anazungumzia jinsi alivyopata huduma ya IRUWASA mwaka 2017 akisema; “Ilichukua wiki moja tu kuingiziwa huduma ya maji nyumbani kwangu na kuondokana na matumizi ya maji ya mabondeni.”
Naye Sophia Mwinuka na Fatuma Juma wa Mtaa Kitasengwa wanasema jamii ya walemavu kama ilivyo wao wamekuwa wakiathirika zaidi na vyanzo vya maji vya mbali na visivyo salama lakini tangu IRUWASA wasogeze huduma katika makazi yao,wanafurahia huduma hiyo kwa saa 24.
Sophia Mwinuka akipata huduma nje ya nyumba yake
Kwa upande wake, Regina Victorine, mkazi wa Don Bosco anasema; “Huduma ya uhakika ya maji nayopata kutoka IRUWASA imeniwezesha kukuza shughuli zangu za ufugaji na hivyo kuniongezea kipato.”
Regina Victorine
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kinegamgosi A, Tatu Alli anazungumzia jinsi kituo cha maji kilichojengwa na IRUWASA katika mtaa huo wa mlimani kinavyowanufaisha wakazi wake.
“Kituo hiki kinachotumia mita ya luku tunakiendesha kibiashara, tunauza maji kwa wananchi wa mtaani ambao hawajaunganishamaji katika nyumba zao na fedha tunazopata tunatumia kumlipa msimamizi wa kituo na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika mtaa wetu,” anasema.
Naye Winfrida Alphonce anajivunia mafanikio ya maisha aliyoyapata kupitia kituo chake cha kuoshea magari cha Kibwawa akisema kama kisingefikiwa na maji ya IRUWASA asingekuwa na uhakika wa kipato kilichomuwezesha kujenga nyumba na kulipa kodi, kusomesha watoto na kupata huduma nyingine muhimu za familia.
“Kwa siku naosha gari tano hadi kumi kwa wastani wa Sh 5,000 na Sh 10,000 kwa gari moja. Kwa gari dogo natumia chini ya unit moja ya maji na gari kubwa unit moja ya maji,” anasema huku akitoa wito kwa wananchi kusaidiana serikali kulinda vyanzo vya maji ili huduma ya IRUWASA iwe endelevu kwa miaka yote.
Winfrida Alphonce akiosha gari katika kituo chake
Akitoa mchanganuo wa gharama za kununua maji Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Oscar Salingwa anasema mamlaka yao inauza unit moja ya maji ambayo ni sawa na lita 1,000 kwa Sh 1,920 tu.
“Kiasi hicho cha maji ni sawa na ndoo 50 za lita 20 au mapipa matano ya lita 200. Ukifanya mchanganuo utaona lita moja inauzwa kwa wastani Sh mbili, ndoo moja Sh 38 na pipa moja Sh 384, viwango ambavyo mwananchi wa kawaida anamudu ikilinganishwa na maji ya viwandani tunayonunua kwa wasatani wa Sh 1,000 kwa chupa ya lita 1.5,” anasema.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Oscar Salingwa
Akizungumzia mfumo wa uchakataji wa ankara za wateja na kulipia bili, Salingwa anasema mfumo wa kuchakata bili unaotumika ni “Unified Majis Billing Sytem” ambao huwezesha wateja kutumiwa bili zao kwa njia ya ujumbe wa simu na ankara za karatasi kwa baadhi ya wateja wa taasisi.
“Wateja wanalipia ankara zao kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ikiwemo M-PESA, TIGOPESA, na kupitia benki za CRDB, NMB, NBC na Benki ya Posta Pia mawakala wa Benki zote hivyo kuwawezesha popote watakapokuwa kulipa bili zao,” anasema.
Anasema kwa wastani Mamlaka inasambaza ankara zenye thamani ya wastani wa Sh Milioni 750 hadi Sh Milioni 800 kwa mwezi na inakusanya wastani wa asilimia 96 ya mauzo kwa mwezi.
“Kiwango hiki cha ukusanyaji kinaiwezesha mamlaka kugharamia shughuli zote za uendeshaji na matengenezo na kuchangia uwekezaji kwenye miundombinu kwa zaidi ya asilimia 35 ya mapato yote,” anasema.
Anasema ili kuboresha huduma kwa wateja, IRUWASA inatoa huduma kwa mujibu wa Mkataba wa Huduma kwa Mteja, ina namba za simu ambazo mteja anapiga bila malipo ili kupata au kutoa taarifa mbalimbali.