Ishu ya pambano la Mwakinyo kuyeyuka ipo hivi

DAR ES SALAAM: Mashabiki wa Masumbwi usiku wa kuamkia leo wamebaki njiapanda baada ya pambano la Bondia Hassan Mwakinyo na Patrick Allotey kuota mbawa.

Dalili ya mvua ni mawingu kwani kabla ya tukio hilo kulianza kuonekana viashiria vya mambo kutokuwa sawa na kusababisha pambano la pili kutoka mwisho lililowakutanisha Haruna Swanga na Ashraf Suleiman kuchelewa na kuacha maswali mengi kwa waliokesha kusubiri pambano hilo.

Hata hivyo baada ya pambano hilo Bondia Ashraf alisema pambano lilichelewa kutokana na kutokubaliana suala la malipo hali iliyomtoa mchezoni na anaamini ndio sababu ya kupoteza pambano.

Baada ya tukio hilo pambano lililolikuwa likifuata ni la Mwakinyo ambapo watu walisubiri kwa muda mrefu bila kuwaona mabondia,

Subra ilivuta kheri , tabasamu lilerejea kwa wapenda ndondi walipomuona Hassan Mwakinyo amefika ulingoni, ila kwa namna alivyoingia haijazoeleka hivyo kulikoni?

Bondia Patrick Allotey alipoitwa ulingoni alijikongoja kiasi na alipofika alifika kama shabiki tuu bila kuvalia kimchezo na hapa ndipo harufu ya pambano kutoweka ilipokolea ukumbini.

Kwa mujibu wa Mwakinyo pambano hilo lilipaswa kusimamiwa na Rais wa WBO ambaye isivyo bahati kumekuwa na changamoto kwenye malipo yake licha ya Rais huyo kuwepo Dar es Salaam.

‘Champez’ aliongeza kuwa kilichokwamisha ni changamoto ya upatikanaji wa malipo yake jambo lililosababishwa na kukosekana kwa Dola lakini fedha hizo zilipopatikana Rais huyo alitafutwa lakini simu yake haikupatikana.

Ikumbukwe siku chache zilizopita Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini (TPBRC), ilisimamisha pambano hilo wakieleza kuwa kumekuwa na uvunjaji wa mikataba na vigezo na masharti na kuacha watu njiapanda kwani promota wa pambano alisisitiza uwepo wa pambano hilo hadi kufikia lililotokea usiku wa kuamkia leo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button